Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufaransa kuwapiga marufuku wanawake wawili kuvaa baibui ni ukiukaji wa haki: UN

Niqab au Baibui ni vazi la kiislamu linalovaliwa na wanawake  na linafunika mwili mzima, na kuacha sehemu ndogo tu ya macho.Yemen, 2007
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Niqab au Baibui ni vazi la kiislamu linalovaliwa na wanawake na linafunika mwili mzima, na kuacha sehemu ndogo tu ya macho.Yemen, 2007

Ufaransa kuwapiga marufuku wanawake wawili kuvaa baibui ni ukiukaji wa haki: UN

Haki za binadamu

Kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imebaini kwamba Ufaransa ilikiuka  haki za bindamu za wanawake wawili, pale ilipowalipisha faini kwa kuvaa baibui, vazi la kiislamu linalofunika mwili mzima.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis, malalamiko mawili yaliwasilishwa mwaka 2016  , baada ya wanawake wawili wa Kifaransa kushtakiwa na kuhukumiwa  kwa kosa la  kuvaa nguo ambazo zinafunika nyuso zao hadharani.

Mwaka 2010 Ufaransa ilipitisha sharia ambayo ina pinga mtu yeyote kuvaa hadharani mavazi ambayo yanafunika nyuso zao.

Mwenyekiti wa kamati Yuval Shany, amesema sharia ya Ufaransa ya kupiga marufuku mavazi hayo imekiuka haki ya uhuru wa dini na Imani kwa wanawake hao na kwamba haikutoa fursa ya mizania yenye manufaa kwa jamii na haki za mtu binafsi.

Kamati hiyo haikuridhishwa  na madai ya Ufaransa kuwa marufuku hiyo ilikuwa ni lazima kutokana na masuala ya   usalama. Kamati ilikubali kuwa dola laweza kumtaka mtu binafsi kuonyesha sura yake katika mazingira yanayohitajika,lakini iliona kuwa marufuku kwa ujumla kuhusu vazi la baibui haikufaa kwa sababu serikali ilizotoa.

Pia kamati hiyo ilibaini kuwa badala ya kuwalinda wanawake ambao wamejifunika mwili mzima, inaweza kuwa na athari ambazo hazikunuiwa kama vile  kubaki majumbani mwao na hivyo kukwamisha hatua zao za kuweza kupata huduma kadhaa za umma  na kujikuta wametengwa.

Sasa kilichobaki ni Ufaransa kutumia muda uliobaki wa siku 180 kwenda kwa kamati hiyo kuieleza hatua ambayo imeichukua kutokana na uamuzi huo wa kamati ikiwemo kulipa fidia walalamikaji na hatua zingine ambazo zitaweza  kuzuia visa kama hicho kutotokea tena hapo baadaye.