Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baa la njaa lanyemelea Yemen- OCHA

Vijana wa kiume wakiwa wamesimama katika jengo lililobomolewa sehemu za Saada Yemen.
WFP/Jonathan Dumont
Vijana wa kiume wakiwa wamesimama katika jengo lililobomolewa sehemu za Saada Yemen.

Baa la njaa lanyemelea Yemen- OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock amesema baa la njaa linanyemelea Yemen, nchi ambayo hivi sasa takribani nusu ya watu wake hawana chakula cha kutosha.

Bwana Lowcock amesema hayo leo mjini New York, Marekani akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kujadili  hali ya kibinadamu nchini Yemen.

Amewaambia wajumbe kuwa, “tahadhari niliyotoa hapa mbele  yenu tarehe 21 mwezi Septemba mwaka huu kuhusu hatari ya Yemen kutumbukia kwenye baada la njaa sasa kinatimia,” akiongea kuwa “tangu wakati huo hali imekuwa mbaya zaidi na leo hotuba yangu itaangazia hatari ya baa la njaa.”

Bwana Lowcock amesema baa la njaa ni kitu nadra sana katika dunia ya sasa ingawa kwa Yemen hivi sasa kuna hatari ya kutangaza baa la njaa.

Amesema baa la njaa linatangazwa kwa kuzingatia vigezo vitatu ambayo ni ukosefu wa  uhakika wa chakula, unyafuzi na idadi ya vifo vya watu vigezo ambavyo anasema kwa Yemen ni dhahiri.

“Angalau kaya moja kati ya tano zina uhaba mkubwa wa chakula, zaidi ya asilimia 30 ya watoto wenye  umri wa chini ya miaka mitano wana unyafuzi na angalau watu wawili kati ya watu 10,000 anafariki dunia kila siku,” amesema mkuu huyo wa OCHA.