Vita dhidi ya ugaidi sio sababu ya kubinya uhuru wa dini au imani:Shaheed

Haki ya uhuru wa dini au imani ni suala mtambuka ambalo mara nyingi halieleweki vyema na kusababisha haki hiyo kukiukwa kwa kiasi kikubwa kote duniani.
Kauli hiyo imetolewa na Ahmed Shaheed , mtaalamu maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya dini au imani. Akizungumza na UN News kuhusu umuhimu wa utekelezaji haki hiyo Bwana. Shaheed amesema hii
(SAUTI YA AHMED SHAHEED )
“Ni haki ya binadamu ya kimataifa na hivyo ni watu binafsi au makundi ya watu ndio ambao wanastahili , hailindi dini pekee. Kila mtu ana haki ya uhuru wa mawazo, dhamiri, dini au imani, na haki hii inajumuisha waaminio, wasioamini, pamoja na imani zisizo za kidini.”
Amesema haki hiyo haipaswi kukiukwa isipokuwa tu kwa misingi ya kuhatarisha usalama wa umma, kuvunja ulutivu, kuhatarisha afya ya umma, kukiuka maadili na kwa kutolinda haki za wengine. Hata hivyo amesema hivi sasa kuna sababu nyingi zichangiazo kukiukwa kwa kiasi kikubwa kwa haki ya uhuru wa dini na Imani, mfano kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi
(SAUTI YA AHMED SHAHEED )
Hii ni kwa sababu nchi nyingi zinatumia uhalali wa hofu kuhusu ugaidi iliyopo miongoni mwa jamii kuwalenga kwa kiasi kikubwa watu au jamii ambazo hawazipendi, wanazozikosoa, zilizo muhimu, au labda wapinzani, hii ni ukiukwaji wa makusudi wa haki hii.
Ameongeza kuwa haiwezekani kujenga jamii huru ambayo ndio kiini cha haki za binadamu bila kuheshimu haki ya uhuru wa dini au Imani. Na kwa mantiki hiyo amekumbusha kuwa
(SAUTI YA AHMED SHAHEED )
“Kuheshimu uhuru wa dini au Imani kwa kiasi kikubwa kunaunda msingi wa mwanzo wa hisia kwa watu binafsi au jamii kuunga mkono haki za binadamu.”