Elimu ndio ufunguo wa Kajiado Kenya-mbunge Kanchory

24 Oktoba 2018

Elimu nimeona kuwa ni ufunguo na ndio maana nikaamua kuipa kipaumbele katika kaunti ya Kajiado ya Kati nchini Kenya, amesema mbunge wa eneo bunge hilo Memusi Kanchory.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, kandoni mwa mikutano ya Baraza Kuu inayoendelea bwana Kanchory amesema, ili kufanikisha lengo namba nne la malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa  lihusulo elimu, na kuhakikisha hakuna mtoto anayesalia nyumba ifikapo 2030, mikakati kabambe imewekwa.

“Kwa sababu eneo la Kajiado ya Kati ni kubwa sana kuna watoto ambao wako mbali sana na shule ka hiyo nimejenga mabweni, hali ambayo imesaidia kwa ajili ya watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kuja shuleni na hivyo basi muda ambao walikuwa wanatumia kutembea wanakuwa wako pale shuleni na kuendelea na masomo yao.”

Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanyika kukabili vikwazo vyote vinavyoweza kumkosesha elimu mtoto kama viko kupiga vita vitendo vya ukeketaji bado ni changamoto kwani 

“Unapata(kuta) kwamba wazazi wanatafuta mbinu za kuwakeketa watoto wao na hii inachangia kurudisha elimu nyumba kwa sababu wasichana wakishakeketwa wanachukuliwa kama wanawake na baada ya muda mfupi wanalazimika kutoka shuleni kwa sababu ya mimba za utotoni, bado ni changamoto, na serikali na sisi kama viongozi tunakabiliana na changamoto hiyo na kuelimisha jamii kuepukana na mila hizo zilizopitwa na wakati.”

Ameongeza kwamba wanatoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kama njia ya kushawishi wazazi kutilia maanani suala hilo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter