Suluhu ya kudumu yasakwa dhidi ya kasi ya ukuaji wa miji Somalia

22 Oktoba 2018

Huko mjini Mogadishu nchini Somalia, kumefanyika mkutano wenye lengo la kusaka suluhu ya kudumu ya kasi kubwa ya ukuaji wa miji kwenye nchi hiyo ya pembe ya Afrika.

Washiriki ni pamoja na maafisa wa serikali za mitaa, Umoja wa Mataifa na serikali kuu ambapo mshauri maalum wa Umoja wa mataifa Walter Kaelin amesema changamoto moto kubwa ya ukuaji wa miji inachochewa pia na urejeaji wa wasomali kutoka ukimbizini na raia kuhama kutoka vijijini kwenye mijini.

Bwana Kaelin amesema, “wasomali milioni 2.6 ni wakimbizi wa ndani hivi sasa na hii ni idadi kubwa kwa kuzingatia idadi ya raia wa Somalia. Hii ni changamoto kubwa ya kibinadamu lakini pia inaathiri maendeleo ya nchi, usalama na pia ujenzi wa taifa hili.”

Akiwa ni mshauri kuhusu masuala ya wakimbizi wa ndani kwa Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Peter de Clercq, Bwana Kaelin amewaambia wataalamu wa mkutano huo uliokuwa unasaka jawabu la ukimbizi mijini ya kwamba iwapo hakuna suluhu ya kudumu ya suala hilo, itakuwa vigumu kwa Somalia kusonga mbele.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP nchini Somalia George Conway, amesema “ni suala la kuangazia wimbi la ukimbizi wa ndani kwa muda mrefu kama sehemu ya ukuaji wa miji na suala hilo litaendelea.”

Amesema ukweli ni kwamba mwelekeo wa uhamaji kutoka vijijini kwenye mijini nao utaendelea na ni vyema kuweka mikakati ya kupanua makazi mijini sambamba na huduma za kijamii.

Tayari Umoja wa Mataifa na wadau wake ikiwemo serikali kuu ya Somalia wanatekeleza mradi wa suluhu za kudumu uliozinduliwa mwaka 2015 ukilenga kupatia suluhu za kudumu ukuaji wa miji.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nchini Somalia, zaidi  ya watu milioni moja, wakiwemo wanawake, wanaume na watoto wanaishi kwenye mazingira ya muda yasiyo salama kwenye nchi hiyo ambayo iligubikwa kwa mzozo wa wenyewe kwa wenyewe kwa miaka kadhaa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud