Hali mbaya katika makazi duni ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu: UN

Maisha ya kila siku ya wakazi wa maeneo duni kama hawa Sujat Nagar mjini Dhaka, Banghladesh
Dominic Chavez/World Bank
Maisha ya kila siku ya wakazi wa maeneo duni kama hawa Sujat Nagar mjini Dhaka, Banghladesh

Hali mbaya katika makazi duni ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu: UN

Haki za binadamu

 Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya nyumba amesema kupuuza  watu takriban milioni 900 wanaoishi katika makazi duni yaliyofurika pomoni ni kashfa kubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu duniani kote ambayo bado inaendelea kupuuzwa na hivyo amezitaka serikali kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Katika ripoti aliyoiwasilisha kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  mjini New York nchini Marekani, Bi Leilani Farha, anasema “hali ya maisha katika maeneo yanayokaliwa na watu maskini si ya kibinadamu ikighubikwa na mrundikano, ukosefu wa huduma za msingi kama vyoo na maji, na kutokuwepo usalama”. Ameongeza kuwa watu wengi wanaishi wa hofuya nyumba zao kubomolewa au kusambaratishwa kabisa wakati wowote.

Farha akielezea changamoto kubwa za nyumba  barani Afrika pamoja na Asia amesema“Katika miji mingi Afrika , zaidi ya nusu ya idadi ya watu huishi katika makazi yasiyo rasmi, na bara la Asia  nako  kuna wakazi milioni 520 wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi, na mara nyingi makazi hayo yapo katika maeneo hatariya kukumbwa na mafuriko au maporomoko ya udongo na yaliyo machafu na machafu.

 Amesema hali hii sio tu kwa mataifa yenye kipato kidogo lakini pia na mataifa yaliyoendelea akitoa mfano wa mataifa ya Amerika kaskazini ambapo alishuhudiamwenyewe watu wakiishi chini ya barabara kubwa bila huduma muhimu kama vyoo na mahemayao yakiwa chakavu kana kwamba yatasambaratika wakati wowote.

Ripoti imeyataka mataifa kutowanyanyapaa watu wa makazi duni na badala yake wasaidie jamii kupata makazi bora  , akisema ,” azma ya mataifa kuhusu ajenda ya maendeleo endelevu ni kutoa nyumba za kutosha na zinazofaa kwa wanadamu na pia kuboresha  makazi hayo ifikapo mwaka 2030 na azma hii ni sharti itekelezwe kama mkakati  wa haki za binadamu.

Ripoti hiyo ina mapendekezo13 ya kuweza kuboresha  makazi hayo duni ili kwenda sanjari na haki ya mtu kupata nyumba pamoja na haki zingine za binadamu.