Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipofanikiwa Afrika, hatutafanikiwa popote pale- Bi. Espinosa

María Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN /Ariana Lindquist
María Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Tusipofanikiwa Afrika, hatutafanikiwa popote pale- Bi. Espinosa

Ukuaji wa Kiuchumi

Mijadala kuhusu Afrika ikitamatishwa hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, hii leo Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wamefanya mjadala wa wazi kuhusu utekelezaji wa ubia mpya wa maendeleo barani Afrika, NEPAD sambamba na ushirikiano wa kimataifa. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

Mjadala huo umeongozwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa María Fernanda Espinosa ambaye amesema ni dhahiri kuwa ushirikiano kati ya Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa ni thabiti zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule.

Amesema uthabiti huu  wa ushirikiano una manufaa kwa pande zote mbili akitolea mfano mfumo wa ushirikiano kwa amani na usalama ambao amesema unafanikisha utekelezaji wa ajenda za Umoja wa Mataifa kwenye utekelezaji wa ulinzi wa amani.

Bi. Espinosa akiangazia ripoti za Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres juu ya ubia wa AU na UN, amesema, "Ninafurahi kuona kuwa ripoti kuhusu Nepad inaonyesha kuwa nchi za Afrika zinaendelea kutekeleza vyema vipaumbele vyake. Mfano programu ya kuendeleza miundombinu AFrika , inalenga kutatua tatizo  la miundombinu barani humo. Moja ya miradi mikubwa kabisa ya miundombinu ni ile ya barabara kuu za kikanda inayounganisha Ethiopia, Sudan Kusini na Kenya. Ushirikiano huu wa miundombinu unadhihirika kupitia será za biashara.”

Hata hivyo Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema ni lazima wahisani watimize ahadi zao za maendeleo kwa Afrika ili ubia kati ya pande mbili hizo uwe ni wa kweli akieleza kuwa “Afrika ni kitovu ya kila kitu tunachofanya hapa Umoja wa Mataifa,. Hatuwezi kufanikiwa kwingine kokote kule iwapo hatujafanikiwa Afrika.”