Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasaka suluhu la uhaba wa chakula na utapiamlo, Uganda

Sokoni mjini Kampala Uganda
World Bank/Arne Hoel
Sokoni mjini Kampala Uganda

WFP yasaka suluhu la uhaba wa chakula na utapiamlo, Uganda

Afya

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP kwa ubia na Mamlaka ya Jiji Kuu la Kampala (KCCA), wameanzisha juhudi za kushughulikia tatizo la uhaba wa chakula na utapiamlo unaoongezeka katika wilaya ya Kampala ambayo ni sehemu ya kati mwa mji mkuu wa Uganda. 

Mkataba wa makubaliano ya ubia huo umetiiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Jiji Kuu la Kampala (KCCA), Jenifer Musisi na Mkurugenzi wa WFP nchini Uganda El Khidir Daloum mjini Kampala.

Wametangaza kuwa tayari wanatafiti kiwango na aina ya utapiamlo na uhaba wa chakula katika wilaya hiyo, kupitia kitengo cha Afya ya Umaa cha Chuo Kikuu cha Makerere.

Bwana Daloum amesema ubia huu utaisaidia juhudi za serikali ya  Uganda kufikia Malengo muhimu ya Maendeleo Eldelevu (SDGs), hasa lile la kutokomeza njaa hadi sifuri, ikizingatiwa kuwa Kampala inachangia asilimia 60 ya pato la ndani la taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya jiji kuu Kampala, Jenifer Musisi amesema waliomba WFP kusaidia katika utafiti huo kutokana na utalamu wao kuhusiana na tafiti za lishe duniani kote ikiwemo wa hivi karibuni Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Watu wengi wamekuwa wakiingia mjini Kampala wakisaka nafasi za ajira lakini wanajikuta katika makazi ambako huduma za msingi na usafi duni, hali inayotumbukiza watoto wao katika magonjwa mbalimbali.

Na kwa mantiki hiyo, utafiti huu utachunguza jinsi gani umaskini na ukuaji haraka wa miji unavyoathiri  usalama wa chakula au utapiamlo niongoni mwa waliomaskini.

Utafiti kuhusu hali ya watu na afya wa kitaifa wa mwaka 2016 unaonesha kuwa kiwango cha utapiamlo miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5 mjini Kampala kiliongezeka kutoka kwa asilimia 13.5 mwaka 2011 hadi asilimia 18 mwaka 2016.