Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi na Ethiopia tumieni fursa ya kahawa yenu kupendwa zaidi na wanywaji wenye uwezo- Ripoti

Kikombe cha kahawa tayari kunywewa
World Bank
Kikombe cha kahawa tayari kunywewa

Burundi na Ethiopia tumieni fursa ya kahawa yenu kupendwa zaidi na wanywaji wenye uwezo- Ripoti

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakulima wa Buni katika nchi za Ethiopia na Burundi ni lazima watumie fursa iliyopo sasa la kupanuka kwa soko la kahawa hususan kwa watu milioni 500 wanaotumia kinywaji hicho kila siku duniani.

Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema hayo katika ripoti  yake iliyotolewa hii leo huko Geneva, Uswisi ikiangazia sekta ya kilimo cha buni ukanda wa Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo ambayo ni sehemu ya mfululizo wa ripoti zinazoangazia masoko ya bidhaa duniani, imesema ingawa soko la kahawa limeendelea kukua lakini Ethiopia ambako ni asili ya aina ya kahawa ya arabica na Burundi ambako kilimo cha buni kimeshamiri tangu miaka ya 1920 bado zinaweza kuchukua hatua zaidi ili kunufaika na kupanuka na kuimarika kwa soko la zao hilo ili kuwa na hakikisho la upatikanaji wake na pia ubora wake.

Miche ya Buni
FAO
Miche ya Buni

 

Mkurugenzi wa kitengo cha biashara ya kimataifa na bidhaa UNCTAD, Pamela Coke-Hamilton ametolea mfano changamoto ambazo mataifa hayo mawili yanakabiliana nayo na hivyo kushindwa kunufaika ipasavyo na kuendelea kupanuka kwa matumizi ya kahawa kwenye masoko ya hali ya juu.

“Mathalani Burundi kilimo cha buni kimekumbwa na mazingira tete, kutokana na hali ya hewa isiyotabirika, mimea iliyozeeka, idadi kubwa ikiwa ina miaka zaidi ya 40, udongo hauna rutuba bila kusahau ukosefu wa mbinu bora za kilimo na ukosefu wa utulivu wa kisiasa,” amesema Bi. Coke-Hamilton akisema pamoja na mauzo ya chai, mauzo ya kahawa nje ya nchi huchangia asilimia 90 ya mapato ya fedha za kigeni ya Burundi.

Hata hivyo amesema kwa kuwa Burundi imeshadhihirisha kuwa inaweza kuzalisha kahawa bora ambayo inapendwa na wanywaji, “ basi hiki ni kichocheo tosha cha kuimarisha wakulima wadogo kupitia vyama bora zaidi vya ushirika.”

Amepigia chepuo pia uwekezaji wa kibinafsi kupitia ubia kati serikali na wafanyabiashara akisema ushirika huo unapaswa kuimarisha ili sekta ya kilimo cha buni iwe na ushindani zaidi.

 

Kahawa
Kahawa
Kahawa

Kwa upande wa Ethiopia amesema nayo inakabiliwa na mazingira kama ya Burundi, “isipokuwa tatizo ni ukosefu wa uhakika wa ubora wa kahawa inayozalishwa kutokana na wadudu kushambulia mara kwa mara, mbinu duni za kilimo, ukosefu wa mafunzo kwa wakulima na udhaifu katika usimamizi wa mnyonyoro mzima wa thamani kuanzia shambani hadi kwa mnywaji.”

Hata hivyo amesema bado kuna fursa zitakazowezesha Ethiopia kutumia fursa ya sasa ili wakulima waweze kunufaika na hatua ya buni  wanayolima kumfikia mnywaji kwenye masoko ya hali ya juu.