Pande kinzani Comoro epusheni kinachoendelea Anjouan- Guterres

17 Oktoba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza wasiwasi wake kufuatia  mvutano unaozidi kuongezeka huko Anjouan moja ya visiwa vya Comoro, mvutano ambao umeripotiwa kusababisha vifo.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa watu wawili wameuawa kutokana na makabiliano kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa upinzani waliokuwa wamejihami kwa silaha wakati wa maandamano yao kisiwani Anjouan.

Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake amesihi pande zote kuwa na utulivu kwa maslahi ya amani na utulivu kwenye visiwa hivyo vya Comoro.

Amesihi pande zote za kisiasa huko Comoro zirejee kwenye meza ya mazungumzo ambayo yalianzishwa chini ya usuluhishi wa mwakilishi wa ngazi ya juu wa Muungano wa Afrika, Ramtane Lamamra.

Hata hivyo amesihi vyama vya kisiasa na mashirika ya kiraia kutekeleza mikakati ya kujenga imani ili hatimaye kusaidia mchakato wa mazungumzo uwe jumuishi.

Mzozo wa kisiasa huko Anjouan moja ya visiwa vikuu vinne vinavyounda Comoro Kuu, ulianza mwezi julai mwaka huu wakati wa kura ya maoni ambayo ilitamatisha mzunguko wa kushika nafasi ya urais miongoni mwa visiwa hivyo.

Wakazi wa kisiwa cha Anjouan nchini Comoro. Ghasia zinaweza kukwamisha shughuli za maendeleo
UN Environment/Hannah McNeish
Wakazi wa kisiwa cha Anjouan nchini Comoro. Ghasia zinaweza kukwamisha shughuli za maendeleo

Upande wa upinzani ulipinga kura hiyo kwa kile ilichosema kuwa iliona ni mbinu isiyo halali ya Rais wa sasa Azali Assoumani ya kumwezesha kuwania tena urais wa Comoro.

Bwana Assoumani ameongoza Comoro tangu mwaka 1999 hadi 2002 halafu akarejea tena mwaka 2002 hadi 2006 na awamu yake ya tatu ilianza tena mwezi mei mwaka 2016 hadi sasa.

Visiwa vinavyounda Comoro ni Ngazidja au Comoro Kuu, Mohéli, Mayottte na Anjouan.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter