Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza umaskini si msaada ni haki ya msingi- UN

Mwanamke akiwa  anatayarisha akianika keki za udongo ambazo zimekuwa  kama ishara ya Haiti ya kukabiliana na njaa pamoja na umaskani.
UN Photo/Logan Abassi
Mwanamke akiwa anatayarisha akianika keki za udongo ambazo zimekuwa kama ishara ya Haiti ya kukabiliana na njaa pamoja na umaskani.

Kutokomeza umaskini si msaada ni haki ya msingi- UN

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ingawa watu bilioni 1 wamejikwamua na umaskini tangu kufanyika kwa maadhimisho ya kwanza ya kutokomeza umaskini duniani miaka 25 iliyopita, bado watu milioni 700 hawawezi kukimu mahitaji yao ya kila siku.

Katika ujumbe wake wa siku ya kutokomeza umaskini uliotolewa hii leo mjini New York, Marekani, Guterres amesema kuwa  watu hao wasioweza kukimu maisha yao, wengi wao wanaishi kwenye maeneo yenye mizozo, wanashindwa kupata huduma za afya, elimu na fursa za ajira na hivyo hawanufaiki ipasavyo na maendeleo ya kiuchumi, wanawake wakiwa ndio waathirika zaidi.

Guterres amesema mwaka huu ambapo “tunaadhimisha miaka 70 ya tamko la haki za binadamu, hebu na tukumbuke kuwa kutokomeza umaskini si suala la msaada bali ni suala la haki. Kuna uhusiano wa kimsingi kati ya kutokomeza umaskini na kuzingatia haki ya msingi ya kila mtu.”

Ametumia ujumbe huo kupongeza hata hivyo uongozi wa kisiasa, uchumi jumuishi na ushirikiano wa kimataifa kuwa vilikuwa chachu vya kuwanua watu bilioni moja kutoka katika lindi la umaskini.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametilia mkazo suala la kusikiliza sauti za mamilioni ya watu ambao bado wanaishi katika umaskini duniani  kwa kuondoa mifumo inayowakwamisha kushiriki katika shughuli za kijamii.

“Lazima tujenge mfumo wa utandawazi wenye haki ambao unajenga fursa kwa kila mtu na kuhakikisha maendeleo ya teknolojia  yanachochea jitihada zetu za kuondokana na umaskini,”amesema Guterres akiongeza kuwa “katika siku hii ya leo ni vyema kuendeleza ahadi ya ajenda 2030 ya kutokumuacha nyuma mtu yeyote.