Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani mauaji ya Hauwah Mohammed Liman huko Nigeria

Kufuatia shambulio kwenye mji wa Rann, tarehe 1 Machi mwaka 2018 ambako wafanyakazi watatu waliuawa na mmoja alijeruhiwa, ndege ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia  usafirishaji wa anga, UNHAS ilisaidia kusafirisha waathirika.
OCHA / Yasmina Guerda
Kufuatia shambulio kwenye mji wa Rann, tarehe 1 Machi mwaka 2018 ambako wafanyakazi watatu waliuawa na mmoja alijeruhiwa, ndege ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia usafirishaji wa anga, UNHAS ilisaidia kusafirisha waathirika.

UN yalaani mauaji ya Hauwah Mohammed Liman huko Nigeria

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kuchukizwa kwake na kitendo cha kuuzwa kwa mfanyakazi wa kutoa misaada wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC huko kaskazini-mashariki mwa Nigeria siku ya Jumatatu.

Mfanyakazi huyo Hauwa Mohammed Liman, alikuwa anashikiliwa mateka tangu mwezi Machi mwaka huu wa 2018 ambapo yaripotiwa kuwa ameuawa na wale waliokuwa wanamshikilia kufuatia shambulio lililofanywa kwenye eneo la Rann, jimbo la Borno ambako watu wengine waliuawa.

 

Kupitia msemaji wake, Katibu Mkuu amelaani vikali kitendo hicho ambapo pia ametumia fursa hiyo kutuma salamu za rambirambi kwa familia yake, marafiki na jamaa huku akielezea mshikamano wake na Rais na wafanyakazi wa ICRC.

 

“Wahusika wa kitendo hicho lazima wafikishwe mbele ya sheria,” amesema Bwana Guterres akielezea pia hofu  yake kuhusu usalama na ustawi wa mateka wengine ambapo ametaka waachiliwe mara moja.

 

Bwana Guterres amesisitiza kuwa pande zote kwenye mzozo huko Kaskazini-Mashariki kwa Nigeria ni lazima zilinde wafanyakazi wanaotoa misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu ambao wanahitaij misaada hiyo kwenye eneo hilo.

 

Eneo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria limekuwepo kwenye mzozo wa muda mrefu hivi sasa ambapo wapiganaji wa Boko Haram wamekuwa wakitishia watu, wakiwatesa na kuwateka nyara.

 

TAGS: Nigeria, Hawa Mohammed Liman, ICRC