Raia wa DRC wafurumushwa Angola, UNHCR yaingiwa wasiwasi

16 Oktoba 2018

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa-UNHCR lina wasiwasi mkubwa kutokana na wimbi kubwa la idadi ya wakimbizi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wanaorejea nyumbani kufuatia hatua ya serikali ya Angola kufukuza wahamiaji.

Msemaji wa UNHCR Geneva, Uswisi, Babar Baloch amesema raia hao wamekuwa wakirejea katika mkoa wa Kasai nchini DRC na kwamba hofu yao ni uwezekano wa kuibuka kwa mgogoro wa kibinadamu hasa kwenye jimbo la Kasai kati ambako hali tayari ni tete.

Amesema takriban raia 200,000 wamewasili katika jimbo la Kasai pekee na wengine wanaripotiwa kuwasili katika jimbo la Kasai kati ambapo katika mji wa Kamako jimboni Kasai, mpakani na Angola wakimbizi hao waliofurushwa wanakesha nje, wengine kwenye familia za wenyeji, makanisani na hata mitaani.

 

 

Wakimbizi wa Congo wakiwa sehemu ya Lunda Norte, Angola.
Paolo Balladelli/UN Office in Angola.
Wakimbizi wa Congo wakiwa sehemu ya Lunda Norte, Angola.

 

 Raia hao wa DRC walikuwa wakifanya kazi katika machimbo ya madini yasiyo rasmi huko Kaskazini Mashariki mwa Angola, kabla ya kufurushwa na kwamba jana jumatatu ilikuwa ni siku ya mwisho ya wageni kupaswa kuondoka nchini humo.

“ Kuna taarifa za kutokea makabiliano ya nguvu katika sehemu fulani nchini Angola wakati maafisa wa usalama  wakijaribu kutekeleza amri ya kuondoka.Kutokana na muda waliopewa kumalizika. Maelfu ya raia wa DRC wanaorejea nyumbani wako katika upande mwingine wa mpaka na wengine wengi wanaonekana wakitembea kwa miguu wakieleka mpaka wa nchi yao, huku wengine wanawasili  upande wa mpaka wa Angola wakiwa ndani ya magari madogo, mabasi  na malori ambapo kutoka hapo hutembea kwa miguu na kuvuka mpaka wakiwa na chochote kile walichoweza kubeba”.

UNHCR inatoa wito kwa serikali za Angola na DRC zishirikiane ili kuhakikisha mienendo hiyo ya binadamu inafanyika kwa kanuni na kwamba kufukuza idadi kubwa ya watu ni kinyume na chata ya Muungano wa Afrika na hivyo pande zote ziheshimu haki za binadamu.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter