Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanadumaa kutokana na njaa, hii haikubaliki- Guterres

Mtoto mwenye utapiamlo nchini Yemen akiwa na mama yake kwenye hospitali ya Al-Sadaqah mjini Aden
OCHA/Matteo Minasi
Mtoto mwenye utapiamlo nchini Yemen akiwa na mama yake kwenye hospitali ya Al-Sadaqah mjini Aden

Watoto wanadumaa kutokana na njaa, hii haikubaliki- Guterres

Ukuaji wa Kiuchumi

Takriban watoto milioni 155 duniani kote wanakabiliwa na utapiamlo hali ambayo huenda ikasababisha wakadumaa maisha yao yote, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika siku ya chakula duniani hii leo.

Guterres katika ujumbe huo amesema hilo ni jambo la kusikitisha kwa kuwa njaa miongoni mwa watoto husababisha nusu ya vifo vya watoto wote duniani, jambo ambalo amesema haliwezi kuvumilika.

Kama hiyo haitoshi amesema ni ajabu katika dunia hii iliyosheheni vitu lukuki bado mtu mmoja kati ya watu wanane hana chakula cha kutosha na kuongeza kuwa watu milioni 820 bado wanataabika na njaa wengi wao ni wanawake.

Ni kwa mantiki hiyo Guterres amesema katika siku hii ya chakula duniani inayoadhimishwa tarehe 16 ya mwezi wa Oktoba kila mwaka “hebu na tuazimie kuwa na dunia isiyokuwa na njaa, dunia ambayo inafanya kila mtu anapata chakula chenye afya na lishe,” akitaka “mataifa, mashirika, taasisi na mtu binafsi  wote kila mmoja afanye kila liwezekanalo kufanikisha  mfumo wa chakula endelevu.”

Katibu Mkuu amesema ni wakati sasa “wa kurejea azma yetu ya kuheshimu haki ya kila mtu ya kupata chakula na hivyo kutomuacha yoyote nyuma.”

Ujumbe wa siku hii leo ni Vitendo vyetu ni mustakabali wetu, dunia bila njaa mwaka 2030 inawezekana.