Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mavuno ya nafaka yaimarika Uganda, lakini bado kuna changamoto- wakulima

Mavuno ya mahindi yanapaswa kuongezwa thamani ili kusaidia kuongeza kipato kwa mkulima
FAO/Christena Dowsett
Mavuno ya mahindi yanapaswa kuongezwa thamani ili kusaidia kuongeza kipato kwa mkulima

Mavuno ya nafaka yaimarika Uganda, lakini bado kuna changamoto- wakulima

Masuala ya UM

Nchini Uganda hali ya upatikanaji wa chakula  imeonekana kuwa bora zaidi kuliko miaka iliyotangulia kutokana na miradi mbalimbali ikiwemo ule wa serikali wa kutokomeza umaskini kwa kuimarisha sekta ya kilimo. Mwandishi wetu John Kibego kutoka Uganda ametembelea familia moja ili kuweza kuhakikisha kauli hiyo.

Katika kijiji cha KatikakaraII tarafa ya Kyangwali wilayani Kikube, Bwana Haruna Batekaniza ni mkulima akisema kuwa, “mahindi, maharagwe, mihogo, kwangu mimi  naona chakula cha kula hakuna shida yoyote. Mahindi yako mengi sasa hivi”

Mwandishi wetu amemkutana nyumbani akiwa na mkewe akitayarisha chakula cha mchana. Mkewe aitwaye Sylvia Kwera anasema “hakuna njaa.”

Kwa upande wake Atuhura Skovia, mkazi wa mjini Hoima ambaye pia ni mfanyabiashara wa bidhaa za kilimo anasema, “mwaka huu bei ya chakula iko  ya chini chini tena chini sana zaidi. Mtu mwenye mahindi anakupatia ya bure na wewe unampatia maharage ya bure. Kwa hiyo ndivyo tumeishi kwa mwaka huu.”

Hata hivyo amesema hali hiyo haijahakikisha usalama wa chakula hasa kwa watu waishio mijini kwa sababu “ukinunua unga dukani, bado bei iko juu. Ni lazima kiongozi wa familia uongeze akili. Unanunua mahindi, unaenda kusagisha upate nguo ndio unaweza kupata chakula kingi.”

Ingawa mavuno yamekuwa ni mengi, Bwana Batekaniza anasema bado kuna changamoto hasa kuwa na fedha za kununua vifaa vya shule vya watoto ikiwemo vitabu na sare za shule pamoja na mahitaji mengine kama chumvi na sukari.