Ukatili dhidi ya watoto wa Sudan Kusini unatisha

15 Oktoba 2018

Kiwango cha vurugu na ukatili wanachokabiliana nacho watoto wa Sudan Kusini kinatisha, amesema mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya watoto na migogoro ya silaha, Bi. Virginia Gamba.

Hii ni kutokana na ripoti iliyotolewa leo mjini New York, Marekani na ofisi ya Bi. Gamba, ikionyesha kuwa inayoonesha zaidi ya watoto 9,200 walitambuliwa na Umoja wa Mataifa kama waathirika wa ukiukwaji mkubwa wa haki zao katika kipindi cha miaka minne kilichoangaziwa na ripoti hiyo kuanzia Oktoba 2014 hadi Juni mwaka huu wa 2018.

“Ukiukwaji mkubwa dhidi ya haki za watoto ilikuwa ni pamoja na kutekwa kwa minajiri ya kutumiwa katika mapigano, watoto wa kiume na wa kike walioingizwa katika mapigano waliuawa au kuumizwa au kufanyiwa vitendo viovu vya kingono. Watoto wengi pia walitumiwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya wananchi na watoto wengine na hivyo kuleta mzunguko wa vurugu”, Bi Gamba amesema.

Nchini kote Sudan Kusini, zaidi ya watoto 5,700 walithibitishwa kuwa waliwahi kuchukuliwa na kutumikishwa na hivyo kuufanya kuwa ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki.

Kwa kuongezea, takribani watoto 2000 walitekwa na zaidi ya 980 waliuawa au kuumizwa na pande zote mbili yaani vikosi vya serikali na hata makundi ya wapiganaji.

Vitendo viovu vya kingono, vikiwemo dhidi ya watoto, vilitumika kama mbinu ya kivita na kama adhabu.

Baadhi ya watoto walioachiliwa huru na makundi yaliyojihami huko nchini Sudan  Kusini.
UNICEF/Bullen Chol
Baadhi ya watoto walioachiliwa huru na makundi yaliyojihami huko nchini Sudan Kusini.

 

Ripoti pia inasema zaidi ya watoto 650 walithibitika kufanyiwa vitendo vya kingono katika kipindi hicho za utafiti, asilimia 75 ya matukio mengi yakihusisha kubakwa na wartu wengi. Kutokana na kuwa si matukio mengi yaliyoripotiwa, ikiwemo matendo hayo dhidi ya watoto wa kiume, huenda idadi ni kubwa zaidi.

Halikadhalika ripoti hiyo imesema jitihada za kuwalinda watoto kama vile kuutekeleza mpango kazi wa mwaka 2012 ambao SPLA waliuridhia tena mnamo mwa 2014, ulikiukwa kwa kuanza kwa mgogoro ndani ya kipindi cha utafiti.

“Ni muhimu kuangazia ukatili unaofanywa na kuufufua upya mpango kazi uliopo ili kumaliza na kuzuia matendo yote ya kikatili dhidi ya watoto, kama ilivyokuliwa na mamlaka wakati wa ziara yangu ya septemba,” Bi Gamba amesema.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter