Tuzidishe azma ya kupunguza majanga:Guterres.

13 Oktoba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonnio Guterres amesema jamii ya kimataifa iazimie upya kuchukua hatua za kukabiliana na majanga ya asili.

Bwana Guterres amesema hayo katika ujumbe wake wa siku ya kudhibiti majanga duniani leo Oktoba 13 akisema kuwa “majanga ya asili yameacha mamilioni ya watu bila makazi, wakipoteze nyumba, zao na ajira.”

Amesema cha kusikitisha zaidi maadhimisho ya mwaka huu yamekuja siku chache baada ya tetemeko kubwa la ardhi na tsunami huko Indonesia lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 2000.

Bwana Guterres amesema hali hii ni kiashiria dhahiri ya kushirikiana pamoja ili kuwa na suluhu dhidi ya majanga.

 

Indonesian Red Cross
Majeruhi wa tetemeko la arshi la Agosti 5, 2018 Lombok Kaskazini anahamishwa na wafanyakazi wa msalaba mwekundu.

 Katibu Mkuu amesema ingawa majanga huwaacha watu wengi wakiwa hoi bila nyumba wala kazi, lakini ripoti mpya  ya majanga iliyotayarishwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupunguza majanga inasema kuwa, sio mataifa yote hutoa ripoti bayana za hasara za kiuchumi kutokana na majanga makubwa yanayozikabili.

Kwa mantiki hiyo anataka nchi wanachama ziboreshe mifumo yao ya kukusanya takwimu zao za majanga pamoja na kuonyesha hasara ya kiuchumi iliyopatikana.

“Kupima kiwango cha hasara kinaweza pia kuchochea serikali kuchukua hatua zaidi za kufikia malengo ya mfumo wa Sendai wa kupunguza hasara zitokanazo na majanga, mfumo ambao unasaka kupunguza hasara zitokanazo na majanga ifikapo mwaka 2030,” amesema Bwana Guterres.

Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo nchi zitakuwa na  hamasa za kubadili maisha ya wananchi na huchangia pakubwa  katika kuondoa umaskini.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter