Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia kidedea Baraza la Haki za Binadamu

Mjumbe akipigia kura nchi yake wakati wa upigaji kura kuchagua wanachama wapya 18 wa Baraza la Haki za Binadamu, HRC, kuanzia 1 Januari 2019
UN /Manuel Elias
Mjumbe akipigia kura nchi yake wakati wa upigaji kura kuchagua wanachama wapya 18 wa Baraza la Haki za Binadamu, HRC, kuanzia 1 Januari 2019

Somalia kidedea Baraza la Haki za Binadamu

Haki za binadamu

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limefanya kura ya siri ya kuteua wajumbe wapya wa Baraza la Haki za Binadamu, HRC, la chombo hicho.

Wajumbe hao wapya 18 wataanza majukumu yao tarehe 1 Januari mwakani ambapo watahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu na iwapo wanataka wataongeza awamu moja ya mwisho katika chombo hicho cha juu kabisa chenye jukumu la kulinda na kuendeleza haki za binadamu duniani.

UCHAGUZI UNAFANYIKA VIPI

Uchaguzi wa wajumbe hufanyika kila mwaka ambapo katika chombo hicho chenye 47, uwakilishi unagawanywa kwa misingi ya maeneo matano ya kikanda.

Ili nchi iweze kushinda inahitaji angalau kura 97 na kura hizo hupigwa kwa siri kama ilivyofanyika leo. Mwaka huu wa 2018 nchi 18 zinamaliza muda wao tarehe 31 mwezi Disemba mwaka huu ambapo 5 zinatoka Afrika, 5 Asia -Pasifiki, 2 Ulaya Mashariki, 3 Amerika Kusini na Karibea na 3 Ulaya MAgharibi na mataifa mengine.

Ukusanyaji wa kura kutoka kwa wajumbe. Uchaguzi huu umefanyika katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 12 Oktoba 2018
UN /Manuel Elias
Ukusanyaji wa kura kutoka kwa wajumbe. Uchaguzi huu umefanyika katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 12 Oktoba 2018

WALIOIBUKA KIDEDEA NA WALIOMALIZA MUDA WAO NI AKINA NANI?

• Waliochaguliwa mwaka huu: Argentina, Austria, Bahamas, Bahrain, Bangladesh, Bulgaria, Burkina Faso, Cameroon,Jamhuri ya Czech, Denmark, Eritrea, Fiji, India, Italy, Ufilipino, Somalia, Togo na  Uruguay. 

• Wanaoendelea na uanachama: Angola, DRC, Misri, Nigeria, Rwanda, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia, Afghanistan, China, Iraq, Japan, Nepal, Pakistan, Qatar, Saudi Arabia, Croatia, Hungary, Slovakia, Ukraine, Brazil, Chile, Cuba, Mexico, Peru, Australia, Iceland, Spain, Uingereza. 

• Wanaotoka kwa sababu hawakuomba kuendelea awamu ya pili: Belgium, Burundi, Ecuador, Georgia, Kyrgyzstan, Mongolia, Panama, Slovenia na Uswisi.

• Wanaotoka baada ya kutamatisha awamu mbili ambazo ni ukomo: Côte d’Ivoire, Ethiopia, Kenya, Korea Kusini, Falme za Kiarabu, Venezuela na Ujerumani.

MAJUKUMU YA BARAZA 

Baraza lina mamlaka ya kupitisha maazimio, kutuma tume za kusaka ukweli na kuanzisha tume za uchunguzi juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Baraza hili la haki za binadamu linaweza kuteua wataalamu huru juu ya masuala mahsusi. Kwa sasa kuna wataalamu 44 kwenye maudhui kadhaa yakilenga nchi 11. Ambapo kazi yao ni kufuatilia na kutoa ripoti juu ya masuala ya haki za binadamu kama walivyoelekezwa.

Mifumo hii yote inatoa fursa ya kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na kuangaziwa, kujadiliwa na ikiwezaka hatua mahsusi kuchukuliwa.