Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wa vijijini ni msingi kwa maendeleo ya wote- Guterres

Wanawake wa kijijini nchini Nepal wakiwa wamebeba mzigo wa kuni.
FAO/P. Johnson
Wanawake wa kijijini nchini Nepal wakiwa wamebeba mzigo wa kuni.

Wanawake wa vijijini ni msingi kwa maendeleo ya wote- Guterres

Wanawake

Kuwawezesha wanawake na wasichana wa vijijini ni jambo muhimu kwa ajili ya kujenga mstakabali bora kwa kila mtu duniani.

Ni ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika siku ya kimataifa ya wanawake wa vijijini inayoadhimishwa hii leo Oktoba 15.

Hata hivyo amesema ili kuwajengea uwezo makundi hayo ni lazima nchi zichukue hatua ya kuhakikisha kuwa wanawake wa vijijini na wasichana wanafurahia kwa hakika haki zao za binadamu.

Ametaja haki hizo kuwa ni pamoja na uwezo wa kumiliki ardhi, kupata chakula cha kutosha na chenye lishe, maisha yasiyo na aina yoyote ya vurugu, na waweze pia kupata huduma bora ya afya ikiwemo afya ya uzazi bila kusahau  elimu bora na nafuu.

Aidha ujumbe wa Bwana Guterres kwa siku hii umesema, ili kufikia hayo ni lazima uwekezaji, maboresho ya sheria na sera na kuwahusisha wanawake wa vijijini katika maamuzi yanayoathiri maisha yao na kwamba kwa kuwekeza katika ustawi, maisha na uimara wa wanawake na wasichana wa vijijini dunia itafikia maendeleo ya wote.