Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania na siri ya kuwa na uhakika wa chakula

Mkulima katika shamba lake
UNDP Comoros/James Stapley
Mkulima katika shamba lake

Tanzania na siri ya kuwa na uhakika wa chakula

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuelekea siku ya chakula duniani hapo kesho tarehe 16 Oktoba, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limetaja siri ya Tanzania kuwa na uhakika wa chakula wakati huu ambapo ujumbe wa mwaka huu unalenga kutokomeza njaa ifikapo mwaka 2030.

Akihojiwa na Stela Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, UNIC, mwakilishi wa FAO nchini humo Fred Kafeero amesema ingawa kuna maeneo machache yenye uhaba wa chakula hatua hiyo ya Tanzania ni ya kipekee akisema, "hiyo haitokei kimakosa lakini ninafikiri kwa sababu ya sera nzuri na mipango waliyonazo kwa kufanya kazi na serikali za mitaa. Katika nchi hii ugatuzi ni kipengele muhimu ambapo unakuta huduma ya wafanyakazi wa ugani katika sekta ya kilimo inatolewa kwa ngazi ya serikali ya kijiji."

Amesema ingawa bado  kuna changamoto ya kufikisha huduma hizo za ugani katika maenoe yote pia "kuna uhusiano kati ya msisitizao wa serikali kwa upande wa viwanda kwa sababu hivi sasa ndiyo mwelekeo wa serikali, kuwasaidia wakulima kuweza kuongeza thamani na kuchakata kile wanachokizalisha ili wapate kipato ambacho kinaweza kuwafanya wamudu vyakula vingine ambavyo hawawezi kuvizalisha”

 

Bwana Kafeero akaulizwa kuhusu dhima ya vijana katika kutokomeza njaa duniani kwa mujibu wa lengo namba 2 la malengo ya maendeleo endelevu , SDGs ambapo amesema ni muhimu sana akisema kuwa “pale ambapo vijana wameshirikishwa, na tuna mifano mingi kwenye nchi ambayo vijana wameshirikishwa kwenye miradi  ya kilimo. "

Mfugaji wa kuku akiwa kwenye moja ya mabanda  yake.
FAO/Sia Kambou
Mfugaji wa kuku akiwa kwenye moja ya mabanda yake.

Bwana Kafeero ameenda mbali zaidi akisema kuwa "Unaona wameleta mabadiliko makubwa juu ya mtazamo wa kilimo, kwa sababu wanaweza kuzalisha mifugo kidogo iwe kuku au mbuzi, wana ile hamasa ya kuongeza thamani ya kile wanachofanya ili waweze kupata soko zuri. Kwa hiyo ni msingi wa kusongesha ajenda ya lakini suala ni unawashirikisha vipi, lakini katika nchi hii kuna jitihada kubwa za  kufanya hilo.”

.