Saudi Arabia achilia huru wanaotetea haki za wanawake- Wataalam

12 Oktoba 2018

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, wanaihimiza Saudi Arabia iwaachilie huru  mara moja na bila ya masharti yoyote watetezi wote wa haki za binadamu za wanawake wakiwemo watetezi sita wanaoshikiliwa kwa  madai ya kuhusika na utetezi wa haki za binadamu waliofanya kwa amani

Katika taarifa waliyoitoa leo Ijumaa mjini Geneva Uswisi, wataalam hao wamelaani kitendo hicho cha kushikiliwa kwa watetezi hao wakisema lazima mashtaka yao yafutwe.

Watetezi  hao ni Israa Al-Ghomgh aliyekamatwa na kuwekwa ndani mwaka wa 2015 kwa kuhusika katika maandamano ya amani ya kutaka demokrasia mwaka 2011, Samar Badawi, Nassima Al-sadah, Nouf Abdulaziz,  Mayya Al-Zahrani na Hatoon Al Fassi ambao walihusika zaidi na harakati za kupigania haki za wanawake kama vile kupiga kura na pia kuendesha magari, na wamekuwa kizuizini kwa kipindi cha miezi minne.

Wataalam hao wameonyesha wasiwasi wao mkubwa  kuhusu hali ya Bi Al Ghomgham , ambaye kesi yake inasikilizwa na mahakama  maalaum ya mjini Riyadh ya kesi za jinai ambayo iliundwa kwa lengo la kushughulikia kesi zinazohusika na ugaidi.

Wataalamu hao wamesema Bi. Al Ghomgham anashtakiwa  kwa  makosa  yasiyo na msingi wa kisheria na zaidi ya yote hana wakili wakati wa kusikilizwa kesi yake.

Wasiwasi wao mwingine kumhusu Al-Ghogham ni kwamba huenda alilengwa kwa kuwa yeye ni wa jamii ya wachache ya Washia wa Saudi Arabia.

Wataalam hao wameikumbusha serikali ya Saudi Arabia kuwa, “ inawajibika kulinda na kukuza  haki za binadamu za watetezi wa haki za wanawake wakati wakiendesha harakati zao halali na  kwa amani. Katika mazingira ya ubaguzi wa kijinsia uliokithiri, watetezi wa haki za binadamu za wanawake, wanakabiliwa na changamoto kubwa wakati kazi zao zinapopingana na fikra potovu na za kijadi za mwanamke katika jamii.”

Watalaam hao wanasema bado wanawasiliana na  wakuu nchini Saudi Arabia kuhusu kesi hiyo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter