Idadi kubwa ya watoto katika maeneo ya Ebola DRC wamerejea shuleni:UNICEF

12 Oktoba 2018

Mwezi mmoja baada ya kuanza kwa mwaka mpya wa masomo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, asilimia 80 ya watoto wenye umri wa kwenda shule kwenye maeneo ya Beni na Mabalako huko jimbo la Kivu Kaskazini ambayo yalikuwa kitovu cha mlipuko wa sasa wa Ebola, tayari wamerejea shuleni. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema nusu ya wanafunzi hao ni wasichana. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na UNICEF mjini Kinshasa, mji mkuu wa DRC pamoja na miji mingine mitatu, Dakar, New York na Geneva, mwakilishi wa wa shirika hilo nchini DRC, Dkt Gianfranco Rotigliano, amenukuliwa akisema kuwa watoto wote , hata wale ambao wako katika maeneo yenye Ebola wana haki ya kusoma.

Amesema ni kwa kuzingatia hilo, UNICEF inahakikisha kuwa  shule zilizopo maeneo yaliyoathirika zinapatiwa msaada unaohitajika  ili watoto na waalimu waendelee na masomo.

Dkt. Rotigliano amesema pindi watoto wanapojifunza jinsi ya kujiepusha na mlipuko wa Ebola, wanasaidia kuepusha kuenea zaidi kwa ugonjwa huo katika jamii.

Wakati huo huo, msemaji wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Geneva, Uswisi Tarik Jasarevic amesema tarehe 11 mwezi huu kulikuwa na wagonjwa 200 ambapo 125 kati yao walithibitishwa kuwa na Ebola na kwamba hadi sasa watu 125 wamefariki dunia.

Bwana Jasarevic amezungumzia pia chanjo dhidi ya Ebola iliyoanza kutolewa Agosti nane mwaka huu, ambapo amesema inaendelea akiongeza kuwa ...

Watu 15,807 wamepewa chanjo katika maeneo tofauti.”

Hadi sasa UNICEF pamoja na washirika wake wameweza kutoa vifaa  vya usafi kwa shule 365 zilizoko katika eneo la mlipuko, limewapatia mafunzo ya kujikinga dhidi ya Ebola waalimu zaidi ya 3,500 na kuwafikia wanafunzi 69,338 kwa kuwapa ujumbe kuhusu Ebola.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter