Jumuiya ya kimataifa tusiwasahau wakimbizi wa Venezuela:Grandi

10 Oktoba 2018

Maelfu ya wakimbizi wa Venezuela wanavuka mpaka na kuingia Colombia kila siku, wengi wao wakisaka usalama kwa kuhofia maisha yao. Kamishina Mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi akihitimisha ziara yake nchini Colombia ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada kwa wakimbizi hawa

Hapa ni katika kituo cha jamii cha jimbo la Divinia nchini Colombia kwenye mji wa mpakani wa Villa del Rosario. Pilika ni nyingi na wakimbizi wamefurika wakisubiri mlo.

Kuna jiko kubwa ambalo kazi yake ni kuandaa maakuli kwa ajili ya maelfu ya wakimbizi wapya kutoka Venezuela wanaowasili kila uchao. Kituoni hapa Grandi amekutana na wapishi wa kujitolea wanaoandaa mlo kwa  ajili ya wakimbizi.

 

Wahudumu hawa wakujitolea wanatoka nchi zote mbili na hugawa makasha 6000 ya chakula cha bure kwa maelfu ya wakimbizi kila siku. Miongoni mwa wapishi hao ni Irene Navajo naye pia ni mkimbizi kutoka Venezuela

"Natayarisha mbogamboga pamoja na wenzangu , sifanyi kazi hii peke yangu, huduma inapokwisha nasaidia kusafisha uwanja, kupiga deki ndani na kupangapanga vitu.”

 Mbali ya mlo kituo hiki kinatoa huduma za afya, tarifa za kisheria na hata burudani. Kinaendeshwa na kanisa kwa msaada wa UNHCR na wadau wengine. Baada ya kushuhudia huduma hiyo Grandi akafunguka

“Naamini ni mfano unaogusa sana, wa jinsi gani watu wenyewe wanavyokabiliana na hali hii, kuleta msaada, mshikamano, usaidizi wa kisaikolojia, na hata burudani ya muziki, kwa kaka na dada zao ambao wamekubwa na zahma.”

 Grandi yuko katika ziara ya mataifa manne ya Amerika Kusini , Colombia, Argentina, Peru na Equador lengo ni kutathimini mahitaji ya wakimbizi kutoka Venezuela na nchi zinazowahifadhi.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter