Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya miaka 4 hatimaye wakazi wa Ulang wapata chakula cha WFP

Chakula cha msaada kikipakiwa katika malori kutoka Tishale hadi mji wa Malakal, Sudan Kusini.
WFP/Gabriela Vivacqua
Chakula cha msaada kikipakiwa katika malori kutoka Tishale hadi mji wa Malakal, Sudan Kusini.

Baada ya miaka 4 hatimaye wakazi wa Ulang wapata chakula cha WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limefanikiwa kuwafikishia msaada wa chakula wakazi wa kaunti ya Ulang huko Upper Nile nchini Sudan Kusini,ikiwa ni mara ya kwanza tangu mapigano yazuke nchini humo mwezi disemba mwaka 2013.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini  Juba, shirika hilo limesema msafara wenye msaada wa vyakula umefikishwa kwa kutumia boti zilizosafiri kupitia mto Sobat.

WFP inasema hatua hiyo imewezekana baada ya majadiliano na makundi kadhaa kwa lengo la hakikisho la usalama wa kusafirisha bidhaa hizo ili ziwafikie walengwa

Msaada huo wa chakula ni pamoja na zaidi ya tani 700 za chakula na virutubisho kama vile mtama, mafuta ya kukaangia pamoja na unga wa uji wa lishe ambavyo vinawatosheleza watu 40,000 kwa mwezi.

WFP inasema shehena hizo zilipakiwa kutoka kaunti ya Renki huko Upper Nile na ilichukua wiko moja kwa shehena hizo kuwasili Ulang.

Ripoti mpya inayoangazia hali ya chakula kwa kipindi kilichosalia kwa mwaka huu wa 2018  na robo ya kwanza ya mwaka ujao wa 2019 inaonyesha kuwa watu milioni 6.1 Sudan Kusini, ambao ni sawa na zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini humo, wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

 

Tishali likipakuwa mzigo wa chakula cha msaada Sudan Kusini.
WFP/Gabriela Vivacqua
Tishali likipakuwa mzigo wa chakula cha msaada Sudan Kusini.

Mkurugenzi mkazi wa WFP nchini Sudan Kusini, Adnan Khan, amesema kuwa watu milioni kadhaa hawajui watapata wapi mlo ujao, wanahitaji msaada wa kibinadamu wa haraka, na bila msaada huo wanakabiliwa na changamoto kubwa.

Amesema kupata fursa mpya za kuwafikishia chakula kunasaidia kuwafikia watu zaidi na kwa njia nzuri na salama.

WFP inapokosa njia bora ya kufikisha chakula, hutumia ndege na kudondosha shehena za vyakula kwa wahitaji, jambo ambalo shirika hilo linasema  gharama yake ni mara sita zaidi ya gharama ya usafiri wa barabarani au majini.

Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu nchini humo, WFP inatoa msaada wa chakula cha dharura ikiwalenga  watu milioni 5 ikitumia kila njia za usafirishaji kama vile barabara, usafiri wa ndege na wa majini.

WFP inapanga kutoa tani za chakula 6,200 kwa watu takriban 130,000 katika maeneo saba ambayo yamekuwa vigumu kuyafikia ikiwemo Ulang, Luakpiny na Nyirol katika kipindi kijachjo cha miezi 12.