Tunatiwa hofu na kushikiliwa kwa raia wa Colombia nchini Venezuela:UN

9 Oktoba 2018

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema inatiwa hofu na kitendo cha raia 59 wa Colombia kuendelea kushikiliwa mahabusu nchini Venezuela bila kufunguliwa mashitaka yoyote kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis msemaji wa ofisi hiyo Ravina Shamdasani amesema mahabusu hao ambao walikamatwa katika operesheni tofauti za usalama mwishoni mwa wezi Agosti na mapema Septemba mwaka 2016, wamewekwa katika mahabusu moja kwenye kituo cha La Yerguara katikati ya mji wa Caracas.

Ameongeza kuwa hali katika mahabusu hiyo imeelezwa kuwa ni mbaya huku mahabusu wakikosa chakula cha kutosha, maji na madawa muhimu kwa ajili ya afya zao.

Ofisi ya haki za binadamu imeutaka uongozi wa Venezuela kuhakikisha mahabusu wanapata huduma za lazima za afya na katika mfumo mzima wa magereza wafungwa wanahakikishiwa fursa ya huduma za afya na madawa.

Mahabusu hao 59 wanashutumiwa kuwa wanamgambo wa Colombia lakini hadi leo hakuna Ushahidi au mashitaka yaliyofunguliwa dhidi yao na Novemba mwaka 2017  jaji wa Venezuela aliamua kwamba waachiliwe bila masharti laniki serikali haikutekeleza uamuzi huo .

Sasa ofisi ya haki za binadamu inaitaka mamlaka ya Venezuela kutekeleza uamuazi huo wa mahakama na kuwaachilia huru mahabusu hao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud