Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi ndio wanaobeba gharama kubwa kwa kukosa ufadhili:UNHCR

wakimbizi wa Kisomali katika kambi ya Daadab, Kenya.
UN Photo.
wakimbizi wa Kisomali katika kambi ya Daadab, Kenya.

Wakimbizi ndio wanaobeba gharama kubwa kwa kukosa ufadhili:UNHCR

Amani na Usalama

Fedha za ufadhili kwa mamilioni ya watu waliolazimika kukimbia makwao na wasio na utaifa zinazidi kuwa finyu na kuwaacha watu hao wakibeba gharama kubwa ya kutotimiziwa mahitaji yao ya msingi. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na kitengo cha wahisani na huduma ya kukusanya fedha cha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Ripoti hiyo iliyotathimini athari za upungufu wa ufadhili kwa ajili ya wakimbizi na watu waliotawanywa, inasema upungufu wa fedha umesababisha kutokidhi mahitaji yote ya wakimbizi na wasio na utaifa kote duniani na kuwaweka watu hawa na jamii wanazoishi katika hatari kubwa.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu  jumla ya watu milioni 68.5 wameelezwa kulazimika kukimbia makwao na hivyo kufanya ufadhili wa nchi kwa wakimbizi na watu wengine waliotawanywa kuwa katika shinikizo kubwa. Akifafanua kuhusu hali hiyo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva Uswis , msemaji wa UNHCR Babar Baloch amesema kulingana na michango hadi kufikia leo , ufadhili kwa mwaka 2018 utakidhi asilimia 55 tu ya dola bilioni 8.2 zinazohitajika, ukilinganisha na asilimia 56.6 mwaka 2017 na asilimia 58 iliyopatikana mwaka 2016 na kuongeza kuwa

 

Wakimbizi kutoka Burundi wakichota maji DRC
UNHCR/Colin Delfosse
Wakimbizi kutoka Burundi wakichota maji DRC

(SAUTI YA BABAR BALOCH)

“Kwa kifupi , fedha za ufadhili zinaendelea kupungua wakati idadi ya wanaolazimika kufungasha virago duniani kote ikiongezeka.”

 Ripoti inaongeza kuwa athari za upungufu huo kwa wakimbizi ni dhahri

(SAUTI YA BARBAR BALOCH)

Katika hali baada ya hali tunashuhudia ongezeko la utapia mlo, vituo vya afya vikifurika, nyumba na vituo vya malazi vikiadimika, watoto wakirundikana darasani au kukosa shule kabisa, na ongezeko la hofu ya ulinzi na usalama kwa sababu ya upungufu wa wahudumu wa kushughulikia watoto wasio na walezi au waathirika wa ukatili wa kingono.”

Ripoti imezitaja hali za wakimbizi na wakimbizi wa ndani ambazo zimeathirika vibaya na upungufu wa ufadhili kuwa ni pamoja na Burundi, Jamhuri ya Kidekrasia ya Congo DRC, Afghanistan, Sudan Kusini na Somalia.