Serikali sikilizeni watoto wa kike na wapatieni haki zao- Wataalam

9 Oktoba 2018

Kuelekea siku ya mtoto wa kike tarehe 11 mwezi huu wa Oktoba, wataalamu wa haki za binadmu wa Umoja wa Mataifa wametaka serikali kote duniani zisikilize sauti za watoto wa kike na wasichana kama njia mojawapo ya kuwapatia haki zao za msingi.

Wataalamu hao kupitia taarifa yao iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi wamesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa hivi sasa vikwazo lukuki vimezingira kundi hilo na hivyo kuwazuia kustawi licha ya kwamba mataifa kupitia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs wameahidi kuwalinda.

“Mila na tamaduni potofu zinazohusiana na  umri na jinsia mara nyingi zinazuia wasichana kusonga mbele na hivyo ni lazima tutambue mazingira ambamo wanaishi na changamoto wanazokabiliana nazo ili haki zao za kibinadamu ziweze kutimizwa na hatimaye wawezeshwe na wawe wachangiaji kwenye jamii zao,” imesema taarifa hiyo.

Wataalamu hao wamesema kupitia malengo namba 1, 4, 5, 8 na 16, jamii ya kimataifa imeazimia kujenga mazingira ambamo kwayo wasichana wanaweza kukua bila kubaguliwa, kunyanyaswa na ambamo umri na jinsia yao katu havitakuwa vikwazo vya wao kuchanua na kustawi.

UNICEF/UN014189/Sang Mooh
HalimŽ kutoka Chad aliozwa akiwa na umri wa miaka 14. Hakuwahi kwenda shule kabisa, tofauti na kaka zake ambao walipelekwa shuleni. Ndoa za mapema ni moaj ya sababu kuu za umaskini kwenye kijiji chake nchini Chad.

Hata hivyo wamesema ahadi hizo zimesalia ndoto na kuna hatari ya kwamba hata mafanikio yaliyopatiakana yanaweza kufutika, wakisema kuwa “idadi ya watoto wa kike wanaoandikishwa shule ya msingi imeongezeka lakini wanapofikia umri wa barubaru wako hatarini zaidi kuozwa mapema na hivyo elimu inasalia ndoto.”

Kando  ya ndoa za mapema, wataalamu hao wamesema watoto wa kike na wasichana wanakabiliwa na usafirishaji haramu, ukeketaji na hata kukosa  haki ya kujisafi wanapokuwa shuleni pindi wanapokuwa kwenye hedhi.

Kwa mantiki hiyo wataalamu hao wamesema ni lazima kusikiliza kile ambacho watoto wa kike na wasichana wanasema na wapatiwe fursa ili waweze kufanikiwa na haki zao za kibinadamu siyo tu ziheshimiwe bali pia zilindwe na zitimizwe.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud