Skip to main content

Bila kushirikisha wanawake amani itakuwa ndoto Sudan Kusini: Lacroix

Ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu kutoka UN na Muungano wa Afrika wakikaribishwa kwa ngoma na shamrashamra Bentui kaskazini mwa Sudan Kusini
UNMISS/Isaac Billy
Ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu kutoka UN na Muungano wa Afrika wakikaribishwa kwa ngoma na shamrashamra Bentui kaskazini mwa Sudan Kusini

Bila kushirikisha wanawake amani itakuwa ndoto Sudan Kusini: Lacroix

Amani na Usalama

Amani ya kudumu  na endelevu haitopatikana nchini Sudan Kusini endapo jamii hususan wanawake hawatoshirikishwa katika mchakato wa kuileta. Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa operesheni za ulinzi wa Umoja wa Mataifa Jean Pierre Lacroix baada ya kukutana na wanawake wakimbizi wa ndani kwenye eneo la Bentiu nchini humo. 

Katika ziara hiyo nchini Sudan Kusini Lacroix ameambatana na mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na masuala ya wanawake Phumzile Mlambo-Ngcuka, mwakilishi wa Muungano wa Arika AU na mwenyekiti wa mtandao wa wanawake na upatanishi Afrika (FemWise) Specioza Wandira-Kazibwe.

Wanawake wakimbizi hao wa ndani hawakusita kutoa madukuduku yao akiwemo Nyamile Malual Jiech

“Wanawake wanabakwa kila wakati na unakuta wanaowabaka wanawake ni wadogo kuliko umri wa watoto wetu, wakati mwingine unakuta wanaume watano au kumi wamejipanga dhidi ya mwanamke mmoja. Hizo ni changamoto kubwa sana kwetu, tunashukuru kututembelea na tunawaomba mtuletee amani nchini mwetu.”

Baada ya ya kuwasikiliza kwa kina Lacroix akafunguka

"Wanataka sauti zao zisikike, wanataka kuwa sehemu ya mchakato wa kuleta amani katika nchi yao, na huu ni ujumbe tunaoondoka nao, tunaamini kwamba hakutaweza kupatikana amani, na haitokuwa endelevu endapo watu wa nchi hii hususan wanawake hawatoshirikishwa katika mchakato, katika kila ngazi, hakutakuwa na amani endelevu"

Ujumbe wa hali ya juu wa UN na AU ukiwa nchini Sudan Kusini.Mkuu wa masuala ya kulindamani wa UN, Jean-Pirre Lacroix na Mkurugenzi mtaendaji wa UN Women,Phumzile Mlambo-Ngcuka wako Sudan Kusini.
UN Photo/Isaac Billy
Ujumbe wa hali ya juu wa UN na AU ukiwa nchini Sudan Kusini.Mkuu wa masuala ya kulindamani wa UN, Jean-Pirre Lacroix na Mkurugenzi mtaendaji wa UN Women,Phumzile Mlambo-Ngcuka wako Sudan Kusini.

AU imeahidi msaada katika mchakato huo wa amani ikiwa ni pamoja na kupeleka wanawake 100 wapatanishi, na miradi itakayotoa fursa za elimu na ajira, Specioza Kazibwe mwakilishi wa AU akasisitiza umuhimu wa mchango wa wanawake katika mustakhbali wa nchi hiyo

"Na sasa kwamba tuko hapa, na makubaliano yametiwa saini , na machafuko yamepungua , tunataka kutumia fursa hii ili kuwawezesha kuhakikisha kwamba watoto wenu wanakula , kuhakikisha kwamba mna sauti kwa kila kitu kinachotokea katika nchi hii."

Ziara hiyo ya siku tatu inamalizika leo.