Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uonevu kwa watoto shuleni ni mtihani mkubwa: UN

Waelimishaji wa rika wakiigiza uonevu shuleni.
UNICEF/Anush Babajanyan VII Photo
Waelimishaji wa rika wakiigiza uonevu shuleni.

Uonevu kwa watoto shuleni ni mtihani mkubwa: UN

Haki za binadamu

Suala la unyanyasaji au uonevu dhidi ya watoto ni changamoto kubwa ya kimataifa. Na hii leo changamoto hio imepewa uzito mkubwa katika mjadala uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Mjadala huo unaofuatia ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uonevu dhidi ya watoto umejikita katika kutafuta mbinu za kuwalinda watoto dhidi ya uonevu huo hususan mashuleni.

Ukiwa umeandaliwa kwa pamoja na ofisi ya mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusiana na kuwalinda watoto dhidi ya uonevu, uwakilishi wa kudumu wa Mexico na Lithuania kwenye Umoja wa Mataifa , shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na shirika la Umoja wa Mastaifa la elimu , sayansi na utamaduni, UNESCO umetathimini hatua ambazo zimeshapigwa katika kulinda haki za watoto na vilevile kuangalia maeneo ambayo bado yanahitaji jitihada zaidi ili kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya uonevu.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu Bi. Marta Santos Pais amesema tatizo hilo la unyanyasaji kwa watoto ni baya  sana na akatoa mfano wa kuonyesha uzito wa tatizo hilo katika jamii,

“Miaka kadhaa iliyopita kimsingi tulifanya utafiti na UNICEF, kupitia mtandao ili kuelewa jinsi watoto wanavyoitizama hatari hii, tisa kati ya kumi wanaonyesha kuwa hili ni suala nyeti katika maisha yao na theluthi mbili wamewahi kukutana na manyanyaso ya namna fulani, na wengine hawakuwahi kumwambia yeyote Kwa kuwa inachukuliwa manyanyaso hayaepukiki na ni sehemu ya makuzi” 

Aidha amesema kitu muhimu kabisa ambacho watoto zaidi ya asilimia 90 wamesema katika utafiti huo ni kuwa, kulindwa kwa watoto dhidi ya unyanyasaji ni haki muhimu ya binadamu.

Huko Villanueva, Honduras, Darwin,16, anakaa ndani ya darasa alilokuwa akichangia na rafiki yake henry aliejiuwa Septemba 2016. Mwalimu anasema rafiki wa karibu walinyanyaswa na wanafunzi wenzao.
UNICEF/Adriana Zehbrauskas
Huko Villanueva, Honduras, Darwin,16, anakaa ndani ya darasa alilokuwa akichangia na rafiki yake henry aliejiuwa Septemba 2016. Mwalimu anasema rafiki wa karibu walinyanyaswa na wanafunzi wenzao.

 

Mmoja wa watoto waliohudhuria mjadala huo, amewaambia washiriki kuwa, baadhi ya watu wazima wanafikiri kuongelea tu unyanyasaji inatosha, lakini kwa mawazo yake anafikiri muziki unaweza kufikisha ujumbe kirahisi ndiyo maana ameamua kutumia njia hiyo kuelimisha jamii,

“Kila mtu anapenda kusikiliza muziki. Na nilifikiri ikiwa watoto watasikiliza aina ya muziki ninaouandika, italeta tofauti. Unyanyasaji unaweza kuanzia hata katika shule ya awali, baadhi ya watoto wadogo hata wa miaka nane nchini Marekani wamejiua kwasababu ya manyanyaso shuleni, tunahitaji mtazamo chanya katika jamii na siyo mambo hasi. Asanteni nyote kwa kazi kubwa na uungaji mkono kwa suala hili”

Naye Stephen Blight mkuu wa kitengo cha kulinda watoto katika Shirika la UNICEF, amesema tayari kuna hatua wanazifanya kwa kushirikiana na serikali mbalimbali duniani ili kuwalinda watoto.

“Kwanza kutekeleza será na sheria za kuwalinda watoto shuleni, pili kuimarisha uzuiaji na kushughulikia matukio yanapotokea, tatu, kuisihi jamii na kila mtu kushirikiana na wanafunzi wanapozungumzia uonevu mashuleni na katika jamii, nne kuwekeza katika mambo ambayo yanaweza kuwafanya watoto wabakie salama na mwisho kukusanya data kuhusu uonevu mashuleni na tusambaze yale yanayofanikiwa”