Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipochukua hatua sasa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi tutalipa gharama kubwa-UN

Kufuatia ,mabadiliko ya tabianchi ukame wa mara kwa mara unatishia usalama wa chakula kwa mfano hapa ni nchini  Niger
©FAO/Giulio Napolitano
Kufuatia ,mabadiliko ya tabianchi ukame wa mara kwa mara unatishia usalama wa chakula kwa mfano hapa ni nchini Niger

Tusipochukua hatua sasa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi tutalipa gharama kubwa-UN

Tabianchi na mazingira

Mabadiliko ya tabia nchi yana athari na yataendelea kuwa na athari kubwa katika haki mbalimbali za binadamu ikiwemo haki ya kuishi, afya, chakula na maji lakini pia haki ya kuwa na mazingira bora endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa.

Kauli hiyo imetolewa leo na David R. Boyd mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na mazingira, baada ya kutolewa ripoti mpya ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Boyd ameziasa nchi kwamba ni lazima kuchukua hatua sasa kushughulikia mabadiliko ya tabia nchi kuanzia matumizi ya nishati ya umeme wa miale ya jua au sola hadi mifumo ya kilimo inayohimili mabadiliko ya tabia nchi, la sivyo tujiandae na miongo yenye hatari kubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu ambayo gharama yake itakuwa mtihani kuilipa.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabia nchi ni moja ya tishio kubwa kabisa dhidi ya haki za binadamu. Naye katibu mkuu wa shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO, Petteri Taalas akiunga mkono hilo alipozungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis amesema

"Kuna dharura ya hali ya juu, ambapo nchi zinapaswa kutimiza ahadi zao baada ya mkataba wa Paris na hadi sasa hatua iliyopigwa haitoshi kutuelekeza kwenye lengo la kufikia nyuzi joto1.5 au 2. Kwa hiyo ni dhahiri kuna haja ya kuwa na lengo hata kubwa zaidi la kufikia nyuzi joto hata 2”

 Ameongeza kuwa bado fursa ipo ya kudhibiti madhara ya mabadiliko ya tabia nchi lakini dunia inahitaji kubadilika na kubadili kila kitu katika maisha ya kila siku kwani,

“Moja ya masuala makubwa ni kwamba, kutukuwa na watu milioni 420 ambao watanusurika na mateso ya mabadiliko ya tabia nchi endapo tutaweza kudhibiti ongezeko la joto kusalia nyuzi toto 1.5. Na tuna maeneo fulani duniani ambayo ni nyeti sana ,kama nchi za visiwa vidogo , ukanda wa Mediterranea na pia eneo la Afrika Kusini mwa Janga la Sahara ambao tayari wameathirika na watateseka zaidi siku za usoni.”

Amesisitiza kuwa “hii ni changamoto yetu tunazalisha nishati asilimia 85 inayoharibu mazingira na asilimia 15 pekee ndio nishati mbadala, hivyo ni wajibu wetu kukabiliana na hali hii.”