Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia mpya ina manufaa ikitumika ipasavyo-Utafiti wa UN

Wasichana wakijifunza programu mbalimbali na uundaji wa roboti.
Picha na (NAMS)
Wasichana wakijifunza programu mbalimbali na uundaji wa roboti.

Teknolojia mpya ina manufaa ikitumika ipasavyo-Utafiti wa UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti ya umoja wa mataifa kuhusu teknolojia mpya imesema nishati itokanayo na vyanzo visivyoharibu mazingira hadi plastiki zinazooza kwa urahisi, akili bandia na magari ya umeme, vina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wanadamu hususani katika kusongesha jitihada za kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na kuangazia mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo ripoti hiyo iliyozinduliwa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani inasema bila sera sahihi, teknolojia hizo mpya zinaweza kusababisha kutokuwapo kwa usawa na mgawanyiko wa kijamii.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa kutokana na utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa kupitia idara yake ya uchumi na masuala ya kijamii, DESA ikiangazia masuala ya kiuchumi na kijamii ya dunia nzima kwa mwaka 2018,imegundua kuwa tayari teknolojia za nishati salama na mifumo ya bora ya utunzaji nishati tayari zinasaidia mazingira endelevu, na kuzisaidia nchi kuziruka teknolojia zilizopo kwa sasa.

Teknolojia mpya zimewezesha upatikanaji wa dawa na kuboresha maisha ya wale walioko katika mazingira hatarishi mathalani uvumbuzi katika fedha za kidijitali au kimtandao zimefanya huduma za kifedha kufikiwa na mamilioni ya watu katika nchi zinazoendekea.

Utafiti pia umegundua kuwa wakati teknolojia mpya ina nafasi ya kuleta faida kwa watu kiuchumi na kimazingira, ikiwa itaachwa bila kuratibiwa vizuri inaweza kupanua zaidi kutokuwepo kwa usawa ndani ya nchi na kati ya nchi na nchi. Mathalani matumizi ya roboti au mashine miongoni mwa teknolojia nyingine, pamoja na kuleta maendeleo, vinaweza pia wakati huo huo kutengeneza washindi na walioshindwa.

Akizungumzia ripoti hiyo Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema, "Afya bora na maisha marefu, mafanikio kwa wote na mazingira endelevu vyote tunaweza kuvifikia ikiwa tutautumia vizuri mchango wa teknolojia hizi mpya"

Naye Mkuu wa DESA Liu Zhenmin amesema ,”Kuna uharaka mkubwa katika kuharakisha juhudi zetu za kushughulikia mabadiliko ya tabia nchi na kuendeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu," akisisitiza kuwa "Teknolojia mpya zinaweza kutoa ufumbuzi wenye tija."

Bwana Zhenmin amesema si lazima kwamba teknolojia mpya itayafanya maisha kuwa bora akisema kuwa anaendelea na kuongeza kuwa, "wakati zina uwezo mkubwa wa kutupa faida kubwa, teknolojia hizi mpya zisipotumika vyema, zinaweza kuwa na matokeo mabaya kwa jamii"

Utafiti umegundua pia kuwa, wakati nchi, sekta fulani au nafasi fulani inaweza kunufaika na teknolojia mpya, wengine wanaweza kunufaika kwa kiasi kidogo au hata kupoteza kabisa. 

Ripoti inasema kuwa nchi nyingi zinazoendelea bado hazijatumia kisawasawa teknolojia iliyopo na mabadiliko ya teknolojia mpya yamejikita zaidi katika maeneo na nchi chache kwa hiyo wale walioko nyuma kiteknolojia watajikuta inawawia vigumu kuyafikia maendeleo endelevu.