Umoja wa Mataifa uko tayari kuisaidia Haiti-Guterres

7 Oktoba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametuma salamu za pole kwa serikali na watu wa Haiti kufuatia tetemeko la ardhi lililokumba kaskazini magharibi mwa kisiwa hicho.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametuma salamu za pole kwa serikali na watu wa Haiti kufuatia tetemeko la ardhi lililokumba kaskazini magharibi mwa kisiwa hicho.

Tetemeko hilo lenye ukubwa ww 5.9 katika kipimo cha richa limetokea usiku wa kuamkia leo.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Guterres amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kuisaidia Haiti.

“Katibu Mkuu anasikitika kutokana na maisha yaliyopotea na majeraha yaliyosababishwa na tetemeko” imesema taarifa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, tetemeko hilo lililotokea usiku wa jumamosi karibu na Port-de-Pax katika ufukwe wa kaskazini mwa ufukwe wa Haiti, limechukua maisha ya watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya  11 na zaidi ya 100 kujeruhiwa.

Tetemeko hilo limeripotiwa kusikika pia katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, na pia katika nchi jirani ya Jamuhuri ya Dominica na mashariki mwa Cuba.

“Umoja wa Mataifa uko tayari kuisaidia serikali ya Haiti katika jitihada za kukabiliana na janga hili” taarifa imeeleza.

Hili ni tetemeko kubwa zaidi kuipiga Haiti tangu mwaka 2010, wakati kisiwa hicho kidogo kilipopigwa na tetemeko la ukubwa wa richa 7.3 na kuwaathiri takribani watu milioni tatu kwa ujumla.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter