Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi wa disemba ni fursa ya kihistoria kwa DRC-UN

Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa wakiongea na vyombo vya habari walipofika DRC tarehe 5 Oktoba 2018.
MONUSCO/Michael Ali
Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa wakiongea na vyombo vya habari walipofika DRC tarehe 5 Oktoba 2018.

Uchaguzi wa disemba ni fursa ya kihistoria kwa DRC-UN

Amani na Usalama

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamehitimisha ziara yao ya saa 72 nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC na kuahidi kuunga mkono mchakato kuelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi disemba mwaka huu huku wakisihi uchaguzi huo ufanyike kwa uaminifu na amani.

Uchaguzi huo ambao umekuwa unasogezwa mbele sasa unafanyika tarehe 23 disemba, mwaka huu wa 2018. Rais Joseph Kabila ameshatangaza hatagombea katika uchaguzi huu kulingana na katiba ya nchi yake.

Jana Jumamosi, wajumbe hao wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa walikuwa na mkutano muhimu na wa kina na Rais Kabila, mkutano ambao balozi François Delattre, mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa anauita “hatua ya juu zaidi ya ujumbe wa baraza mjini Kinshasa”

“Tumeonesha utayari wa Baraza la Usalama kuungana mkono na DRC kuelekea kwenye amani, usalama na maendeleo,” anasema Delatter, akiongeza kuwa “Uchaguzi wa disemba 23 unaweka fursa ya kihistoria katika njia hii. Wanatengeneza njia ya mabadiliko ya kidemokrasia ya kwanza na amani”

Wajumbe hao walipofika Kinshasa ijumaa mchana, walifanya mkutano wa saa mbili na Tume huru ya uchaguzi ya DRC, CENI, wakijadili maendeleo na changamoto za mchakato wa uchaguzi.

Rais wa CENI, Corneille Nangaa, amelishukuru baraza kwa msaada muhimu wa Umoja wa Mataifa kwa mchakato wa uchaguzi. “Leo tuna zaidi ya wataalamu 130 wa MONUSCO ambao ni washauri wetu” Nangaa aliwaambia wanahabari akiuzungumzia ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC.