Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni yetu dhidi ya Fistula Aweil ni kuwarejeshea hadhi waathirika:UNFPA

Daktari akizungumza na mmoja wa wagonjwa wa Fistula.
UNFPA/Ollivier Girard
Daktari akizungumza na mmoja wa wagonjwa wa Fistula.

Kampeni yetu dhidi ya Fistula Aweil ni kuwarejeshea hadhi waathirika:UNFPA

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA juma hili linahitimisha kampeni ya mwezi mzima iliyoanza Septemba dhidi ya matatizo ya fistula katika eneo la Aweil nchini Sudan Kusini.

UNFPA inasema matatizo hayo huwapata wanawake baada yakuchanika pindi wanapojifungua wakiwa na umri mdogo au kutokana na athari za masuala ya ukeketaji yanayowasababishia wanawake kusalia na kovu .

Akizungumza na Radio Miraya ya Umoja wa Mataifa kuhusu kampeni hiyo afisa wa afya ya uzazi wa UNFPA Luka Lual Aleu amesema  kampeni hiyo inafanyika kwa ushirikiano na wizara ya afya ya serikali ya Sudan kusini na idara ya afya ya jimbo kwa lengo la kuwafanyia upasuaji wanawake manusura wa fistula zaidi ya 40.

Bwana. Aleu ameihimiza jamii ya jimbo la Aweil kuwa kuripoti visa vya fistula katika clikiniki ni muhimu hivyo

“Ujumbe ninaotoa kwa jamii ni kwamba  tunahitaji waathirika zaidi wa fistula kuja , kama una mtu yeyote, mkeo, dada yako, wifi yako , mpeleke kwenye hospital ya Aweil kitengo cha uzazi wa mpango, andikisha majina yao, na tunachukua namba zao za simu , na tunawapigia baada ya kupata ujumbe kutoka Juba lini kampeni kama hii itakuja tena , na tunawapigia kabla wili waje kwenye hospital yetu ya Aweil.”

Na je kuhusu gharama ?

“Upasuaji huu ni bure bila gharama yoyote na malazi pia ni bure , na UNFPA imeamua sasa kutoa msaada wa mafunzo kwa wazazi, watu wanaowasaidia waathirika , na kina mama wenye matatizo ya fistula  kabla ya kurejea katika makazi yao ya kawaida.”

Ameeongeza Fistula ni tatizo la kiafya ambalo limekuwepo kwa muda mrefu na linalotokana na kuwepo kwa tundu kati ya kibofu cha mkojo na njia ya uke au hata na njia ya haja kubwa kwa sababu ya uzazi pingamizi. Wanawake na wasicha walioathirika na tatizo hili hunyanyapaliwa sio tu kimwili na kifikra bali pia katika jamii na baada ya kutengwa hujikuta hawana pa kwenda hivyo huduma kama hizi zinapotokea ni vizuri ili kuwasaidia.