Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtandao wa kijamii umeniwezesha kufika UN- Mshiriki UNRAF

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kati) akiwa na washiriki wa UNRAF 2018. Marygoreth Richard (kulia kwa Katibu Mkuu) ni mshiriki kutoka Tanzania
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kati) akiwa na washiriki wa UNRAF 2018. Marygoreth Richard (kulia kwa Katibu Mkuu) ni mshiriki kutoka Tanzania

Mtandao wa kijamii umeniwezesha kufika UN- Mshiriki UNRAF

Masuala ya UM

Programu ya Umoja wa Mataifa ya kunoa waandishi wa habari kuhusu masuala ya chombo  hicho ikikunja jamvi hii leo, mmoja wa washiriki kutoka Tanzania amezungumzia kile ambacho ataondoka nacho baada ya kuwepo makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa wiki tatu.

 

Akihojiwa na Idhaa  ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Marygoreth wa BBC Media Action Tanzania ambaye ameshiriki programu hiyo ya Reham Al Farah Memorial, UNRAF amesema, " Mimi ingawa niko kama mtayarishaji wa kipindi cha Haba na Haba, najihusisha pia na radio za kijamii, kwa hiyo nitasaidia kuelimisha waandishi wa habari kuhusu kazi za Umoja wa Mataifa na jinsi ambavyo unafanya kazi.

Awali Marygoreth ambaye ni miongoni mwa waandishi wa habari 15 kutoka nchi zinazoendelea walioshiriki mafunzo hayo yaliyowapatia pia fursa ya kuandika habari za mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA alielezea jinsi alivyopata fursa hiyo akisema kuwa, "ilikuwa kupitia mtandao wa kijamii, kuna rafiki  yangu alichapisha akasema kuan hiyo fursa kwenye Umoja wa Mataifa inatokea mara moja kwa mwaka. Nami nikaangalia nikaona inafaa. Lakini nikapitia kwanza kwa kina na nikaona ni lazima nijiandae vyema katika kuweka kila kitu kinachohitajika. Mimi naamini kuwa kila kitu unachotaka ufanikiwe ni lazima ujiandae vyema."

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (kati) akiwa na washriki wa mpango wa UNRAF 2018 kwenye makao makuu ya UU, New York, Marekani
UN /Kim Haughton
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (kati) akiwa na washriki wa mpango wa UNRAF 2018 kwenye makao makuu ya UU, New York, Marekani

UNRAF hufanyika kila mwaka kuanzia mwezi Septemba hadi mwanzoni mwa mwezi Oktoba ambapo waandishi wa habari pamoja na kuripoti habari wakati wa UNGA, hupata fursa ya kuelimishwa jinsi Umoja wa  Mataifa wenye wanachama 193 unafanya kazi zake.

Washiriki wa mwaka huu wametoka, Tanzania, Uganda, Kenya, Kuwait, Burundi, Nicaragua, Sri Lanka, Uturuki, Afghanistan, Venezuela, India, Serbia, Cambodia, Bangladesh na Nigeria.

Programu ya Reham Al-Farrah imepatiwa jina hilo mwaka 2003 kumuenzi mwanahabari Reham, afisa habari wa UN kutoka Jordan ambaye aliuawa kwenye shambulio la bomu dhidi ya ofisi ya Umoja wa Mataifa tarehe 19 Agosti mwaka 2003 huko Baghdad, nchini Iraq.

Awali programu hiyo ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi disemba mwaka 1980 kwa azimio namba 35/201 na  hadi sasa jumla  ya waandishi 581 kutoka mataifa 168 wamenufaika nayo.