Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasaidia Nigeria kukabili athari za mafuriko

Watoto walicheza katika eneo lililokumbwa na mafuriko Maiduguri jimboni Boeno Kaskazini mashariki mwa Nigeria.
UNICEF/Fati Abubakar
Watoto walicheza katika eneo lililokumbwa na mafuriko Maiduguri jimboni Boeno Kaskazini mashariki mwa Nigeria.

WHO yasaidia Nigeria kukabili athari za mafuriko

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO linashirikiana kwa karibu na serikali ya Nigeria ili kukabiliana na madhara yaliyotokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.

Mamlaka ya kitaifa ya masuala ya dharura nchini Nigeria, NEMA inasema hadi sasa mafuriko hayo yaliyokumba majimbo 12 nchini humo yameathiri zaidi ya watu 826,000 huku 199 wakipoteza maisha na wengine zaidi ya 176,000 wamesalia wakimbizi wa ndani.

Majimbo hayo ni  na Adamawa, Anambra, Bayelsa, Benue, Delta, Edo, Kebbi, Kogi, Kwara, Niger, Rivers na Taraba.

Mwakilishi wa WHO nchini Nigeria, Dkt. Wondimagegnehu Alemu amesema kwa kuzingatia uwezo wao wa kitaalamu, shirika hilo linasaidia serikali ya Nigeria na zile za majimbo hayo kutathmini hali ya kiafya na mahitaji.

Dkt. Alemu amesema usadizi huo ni muhimu kwa kuwa “pamoja na kusababisha vifo, mafuriko yanaweza kuleta madhara makubwa ya kiafya kwa jamii hata baada ya maji kutoweka. Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, NEMA na mamlaka ya uchunguzi wa magonjwa ya Nigeria, NCDC, WHO inatoa huduma kama vile maji safi na salama, dawa na makazi.”.

Ameongeza kuwa shirika lake liko tayari kusaidia juhudi za serikali za kupunguza  athari za mafuriko kuhusu afya ya wananchi kwa ushirikiano na serikali kuu pamoja na za majimbo.

Tayari WHO imetuma wataalam wake katika maeneo hayo kama njia ya kuzuia na pia kudhibiti kusambaa kwa magonjwa ya kuambukiza kutokana na mafuriko hayo.

Wataalam hao wanaimarisha uwezo wa kudhibiti na pia kuweka mifumo ya kutoa onyo hususan katika kambi za muda za watu walioachwa bila makazi.

Pia shirika hilo linaisadia serikali kuu kuona kama dawa zinazohitajika pamoja na vifaa vinapatikana na pia kutoa msaada wa vitendea kazi.