Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada zaidi zinahitajika kulinda haki ya kukusanyika na kujumuika Tunisia- Mtaalamu

Mtaani nchini Tunisia mwaka 2016
World Bank/Dana Smillie
Mtaani nchini Tunisia mwaka 2016

Jitihada zaidi zinahitajika kulinda haki ya kukusanyika na kujumuika Tunisia- Mtaalamu

Haki za binadamu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za mikusanyiko ya amani na kujiunga na vyama, Clément Nyaletsossi Voule, ameridhishwa na jitihada za serikali ya Tunisia za kuimarisha demokrasia tangu yalipofanyika mapinduzi mwaka 2011 huku akizisihi mamlaka hizo kuongeza jitihada kulinda haki za mikusanyiko ya amani na kujumuika.

“Tunisia iko katika hatua ya mageuzi katika historia yake ya mapinduzi,” anasema Voule, mwishoni mwa ziara yake ya siku 10 ya kikazi nchini Tunisia. “Ni matumaini yangu kuwa mabadiliko ya kidemokrasia yatadumishwa na yataelekeza katika jamii ya haki na kidemkrasia kwa kuendana na kauli mbiu ya mapinduzi ambayo ni ‘Ajira, Uhuru na Utu’

Bwana Voule amesema“ziara yangu ilikuja muda muafaka, kwa sababu Tunisia imekuwa ikijadili sheria mpya ambazo zitagusa haki na uhuru wa mikusanyiko ya amani na kujumuika. Mikutano yangu na washiriki kadhaa imenifanya kuelewa kuhusu hali ya mpito wa mabadiliko ya kidemokrasia hususani kuhusu kufurahia haki ya uhuru wa kukusanyika kwa amani na kujumuika.” 

Pamoja na kupongeza hatua zilizofikiwa, mtaalamu huyo amezitaka mamlaka zitumie sheria mpya na kuanzisha taasisi kwa kuendana na viwango vya haki za binadamu za kimataifa akitaka zaidi vitendo kuliko maneno.

Aidha mtaalamu huyo aliwataka watunga sheria kuhakikisha kila mtu anakuwa huru kukusanyika na kujumuika.

Ameeleza kuhusu hali ambayo imekuwepo ya kuwakamata watu kiholela na matumizi ya nguvu.

Halikadhalika Voule amezungumzia kuchelewa kuanza kwa taasisi ambazo zilianzishwa na katiba ya mwaka 2014 kama mahakama ya kikatiba, mahakama mpya ya wakaguzi wa fedha ma taasisi ya haki za binadamu. “Bila taasisi hizo, mabadiliko ya kidemokrasia ambayo haki za uhuru wa kukusanyika kwa amani na kujumuika ni nguzo muhimu, haziwezi kuhakikishwa na zinaweza kuminywa” anasema.

Mtalamu huyo huru ametembelea nchi hiyo kufuatia mwaliko wa Tunisia na alikutana na mamlaka za serikali, akiwemo Waziri mkuu na wawakilishi wa taasisi huru. Pia alifanya mikutano na washiriki kadhaa wa mashirika ya kiraia na wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.