Ushirikiano kati ya FAO na EU kuendelea ili kunusuru jamii hususan dhidi ya njaa

App (programu tumizi) mpya inayoongea, inawasaidia wakulima kama Tazelekwew, kusini mwa Ethiopia kufahamu kama mazao yao yameathiriwa na wadudu.
FAO/Tamiru Legesse
App (programu tumizi) mpya inayoongea, inawasaidia wakulima kama Tazelekwew, kusini mwa Ethiopia kufahamu kama mazao yao yameathiriwa na wadudu.

Ushirikiano kati ya FAO na EU kuendelea ili kunusuru jamii hususan dhidi ya njaa

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na Muungano wa Ulaya, EU, leo wamesisitiza kuendeleza ushirikiano kati yao kwa lengo la kushughulikia masuala kama vile kuongezeka kwa njaa na kuleta ustawi na amani sambamab na kujenga jamii endelevu duniani.

Hatua ya leo iliyofikiwa huko Roma, Italia kati ya Mkurugenzi mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva na Kamishna wa ushirikiano wa kimataifa na maendeleo wa EU, Neven Mimica, ni mwendelezo wa ushirikiano kati ya pande mbili hizo ambapo katika miaka kumi iliyopita, EU imechangia zaidi ya Euro bilioni 1.5 katika shughuli za FAO duniani kote.

Mathalani katika kipindi cha miaka miwili ijayo, EU na  FAO watajikita zaidi katika kujenga  uwezo wa jamii kukabiliana na upungufu wa chakula, kujadili masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na matumizi mazuri ya mali asili, kuwekeza katika kilimo na mnyororo wa thamini na kuboresha lishe na mfumo wa chakula.

“Uungaji mkono unaoendelea kufanywa na EU kuhusu ushirikiano miongoni mwa mataifa na Umoja wa Mataifa ni wa muhimu ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu  mwaka 2030 kama ilivyo kuziangazia changamoto kubwa zilizosababisha uhamaji, mgogoro na uhaba wa chakula hii leo” anasema Bwa da Silva.

Ameongeza kuwa “kwa kufanya kazi pamoja na kuunganisha utaalamu wetu, ninashawishika kuwa tunaweza kuzikabili changamoto tulizo nazo.

Kwa upande wake Mimica amesema “Ninajisikia fahari kwa hatua ambayo sisi EU na FAO tumeifikia kwa pamoja. Tunabaki tukifahamu kwa hakika kuwa uhaba wa chakula na kilimo endelevu vinabakia kuwa changamoto kubwa. Ndiyo maana kwa mwezi uliopita pekee, kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, EU na FAO tulitia saini makubaliano ya Euro milioni 77 kwa ajili ya mamilioni ya watu wanaohangaika na uhaba wa chakula duniani kote.

Kati ya mwaka 2007 na 2017, EU ilielekeza zaidi ya Euro bilioni 1.5 katika programu 250 za FAO kwenye nchi 60 ili kusaidia kupambana na uhaba wa chakula na kuaangazia usalama wa chakula pamoja na kuendeleza kilimo kilichoathiriwa na mambo kadha ikiwamo migogoro, kuhama, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.