Tumbaku inaharibu mazingira kuliko ilivyofahamika- Ripoti

2 Oktoba 2018

Suala la matumizi ya tumbaku kuhatarisha afya ya binadamu limekuwa bayana miongo na miongo hata hivyo hii leo ripoti mpya imeweka dhahiri vile ambavyo tumbaku inasabaratisha mazingira.

Ikiwa imeandaliwa na sekretarieti ya mkataba wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya tumbaku, FCTC wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, ripoti hiyo imezinduliwa wakati wa mkutano wa 8 wa nchi wanachama wa mkataba huo, COP8 unaoendelea huko Geneva, Uswisi.

Ripoti hiyo iliyochapishwa leo imeelezea kinagaubaga jinsi uzalishaji na matumizi ya tumbaku vinavyoharibu mazingira na hivyo kutishia kufanikisha maendeleo endelevu.

“Kilimo cha tumbaku kinahitaji eneo kubwa la ardhi, matumizi ya maji mengi na nguvukazi kubwa na rasilimali hizi zote zinaweza kutumiwa katika maeneo yenye tija zaidi. Madhara ya kilimo hiki ni pamoja na ukataji miti unaosababisha mabadiliko ya tabianchi, vyanzo vya maji kukakua na udongo kupoteza rutuba, sumu kumuingia binadamu na udongo kuwa na kiwango kikubwa cha aside,” imesema ripoti hiyo.

Ikilinganisha uharibifu wa mazingira utokanao na tumbaku na mazao mengine, ripoti inasema kuwa ni kubwa na kiwango cha mavuno katika eneo sawa la ardhi kinakuwa ni kidogo kwa zao la tumbaku ikilinganishwa na mazao mengine.

“ Mathalani nchini Zimbabwe eka moja ya ardhi inaweza kuzalisha kiwango cha viazi mara 19 zaidi ikilinganihswa na tani kati ya 1 hadi 1.2 za tumbaku.halikadhalika ushaidi unaonyesha kuwa kupanda mazao mbadala ni bora kwa wakulima na familia zao. Ajira kwa watoto ni tatizo kubwa kwenye kilimo cha tumbaku, ikiathiri afya ya watoto na haki zao ikiwemo kupata elimu.”

Katika kiwango cha mtu mmoja mmoja cha uharibifu wa mazingira, ripoti inasema kuwa katika uhai mzima, mtu anayevuta paketi moja ya sigara yenye sigara 20 kwa siku kwa miaka 50 atakuwa amewajibika na matumizi ya lita milioni 1.4 za maji.

Tumbaku inaharibu mazingira. Picha: WHO/Video capture
Tumbaku inaharibu mazingira. Picha: WHO/Video capture

Ripoti inasema kuwa takribani asilimia 90 ya kilimo cha tumbaku kimejikita katika nchi zinazoendelea, ambapo nchi 10 zinazoongoza kwa uzalishaji wa tumbaku, 9 ni zile zinazoendelea na 4 ni zile za kipato cha chini na zina uhaba wa chakula zikiwemo “India, Zimbabwe, Pakistan na Malawi. Hata hivyo faida ya sekta hii inabakia katika nchi zilizoendelea.”

Dkt. Nicholas Hopkinson, ambaye ni mwandishi mwenza wa ripoti hiyo kutoka Chuo cha National Heart and Lung Institute, Imperial College mjini London, Uingereza, amesema “Kampuni kubwa za tumbaku zina makao yake makuu katika nchi zilizoendelea na zinatumia kiholela rasilimali na mustkhbali wa watu maskini zaidi kwenye sayari ya dunia.”

Ripoti inataka wakulima wa tumbaku wasaidiwe ili waondokane na kilimo cha zao hilo na badala yake wapatiwa zao mbadala ili kupunguza uharibifu wa mazingira katika mashamba yao.

Katibu Mkuu wa sekretarieti ya FCTC Dkt. Vera Luiza da Costa e Silva amesema, “udhibiti wa tumbaku ni suala la maendeleo. Uharibifu wa mazingira unatokea katika mzunguko mzima wa tumbaku kuanzia kilimo ikihusisha ukataji miti, uchafuzi wa maji kutokana na matumizi ya dawa za kuulia wadudu na utupaji wa vishungi vya sigara. Mkataba wa WHO FCTC unaojumuisha zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa binadamu, ni jibu la tatizo hili.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter