Tukiadhimisha siku ya kupinga machafuko, tufuate nyayo za Gandhi- Guterres

2 Oktoba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa dunia kufuata mtazamo na busara za Mahatma Gandhi katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga machafuko ambayo huangukia Oktoba Pili kila mwaka, siku ya kuzaliwa kiongozi huyo mashuhuri wa India aliyehamasisha vuguvugu la haki za kiraia kote duniani.

Akiwa nchini India Katibu Mkuu amesema katika ujumbe wake maalumu wa siku hii kwamba “katika wakati ambao umeghubikwa nan a migogoro na changamoto lukuki , fikra za Gandhi za kupinga machafuko zinasalia kuwa chagizo kubwa”. Ameongeza kuwa mfano wa Gandhi unaonyesha kuwa njia pekee ya kufikia malengo ni kuepusha machafuko, na kwamba “ninaweza tu kutumai kwamba wale wote walio na majukumu ya kisiasa duniani wanaweza kuwa na thamani kama ya Mahatma Ghandhi na kuelewa kwamba wanapaswa kufikia malengo yao kupitia majadiliano, kupitia kutokuwa na machafuko, kwa kuwa na dhamira ya kweli kwa mustakabali wa watu wao.”

Kwa Umoja wa Mataifa amesema , dunia bila machafuko na kutatua tofauti kwa njia ya Amani inamaanisha ni kitovu cha kazi ya Umoja huo.

Akikumbusha kuhusu dhamira ya Gandhi ya kuhakikisha haki ya kijamii kwa wote , Guterres amesema wakati huu ambapo pengo la kutokuwepo usawa likiongezeka ni muhimu kuwa na mchakato wa utandawazi ulio sawia kwa kuzingatia utu wa binadamu hasa dunia iking’ang’ana kufikia malengo n ya maendeleo endelevu SDGs  na kuhakikisha usawa wa kijinsia na kutomuacha yeyote nyuma.

Kama alivyoamini Gandhi, Guterres amesema “kuepuka machafuko katika kushughulikia vitosho vya amani , ni msukumo mkubwa kwa binadamu.”

Akiweka shada la mau katika makumbusho ya Raj Ghat mjini New delhi katika kumuenzi Gandhi katika miaka 150 ya kuzaliwa kwake Guterres ametoa wito kwa dunia kuhamasishwa na ujasiri na dhamira ya mwanaharakati huyo wakati juhudi zikiendelea katika kudumisha amani, malengo ya maendeleo endelevu na haki za binadamu kwa wote.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter