Tuimarishe ushirikiano wa kimataifa ili kunusuru uhamiaji- Grandi
Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi ametoa wito kwa mataifa kushirikiana ili kupata ufumbuzi wa suala la wakimbizi akisema makubaliano mapya kuhusu wakimbizi yatageuza hifadhi kuwa jibu mujarabu.
Kamishna Mkuu Grandi, amesema hayo leo mjini Geneva Uswisi, wakati akifungua mkutano wa 69 wa mwaka wa Kamati tendaji ya UNHCR.
Ametaka kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimataifa ili kuweza kukabiliana vilivyo na ongezeko la migogoro inayozidi kupanuka ambayo amesema imewalazimisha watu wengi kuhama makazi yao katika sehemu nyingi duniani.
“Misingi ya ushirikiano wa kimataifa imepata shinikizo kubwa, lakini licha ya hayo ushirika bado umesimama kidete. Lakini ni lazima tuongeze nguvu,” amesema Bwana Grandi akiongeza kuwa tangu achukue hatamu za shirika hilo, mwaka wa 2016, migogoro ya ndani imeongezeka ikichochewa na uhasama wa kikanda na wa kimataifa, na kuongezewa chumvi na umaskini, ubaguzi wa rangi pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Ikiwa hiyo haitoshi amesema kuwa nazo kauli za kisiasa zimekuwa kali na kutoa mwanya kwa ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni.
Grandi akiita tukio muhimu katika ushirikiano mkubwa, amesema kuwa tamko la New York la mwaka wa 2016 kuhusu wakimbizi na wahamiaji, lilidhihirisha azma ya kisiasa ya hali ya juu ambayo inahusu ushirikiano wa kimataifa pamoja na viwango vya kuwalinda wakimbizi.
Pia amekaribisha makubaliano mapya kuhusu uhamiaji ambao utapitishwa baadaye na Baraza Kuu la Umoja waMataifa akisema ni njia mpya na ya wazi ya kuchukua hatua bora.
Ameongeza kuwa, “naamini ni uthabiti wa ushirikiano wa kimataifa- kama ushahidi dhahiri dhidi ya kauli za kichochezi ambazo zinashamiri kwenye majukwaa kuhusu wakimbizi na wahamiaji.”
Akigusia muhula wake jinsi ulivyokuwa Grandi amebaini kuwa migogoro kama ile ya Syria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, na Kaskazini mwa Amerika Kusini imeendelea huku mingine kama vile Yemen, imezidi kupanuka.
Ametaja baadhi ya migogoro kama ile ya Iraq, kanda ya ziwa Chad na Sudan Kusini kama inayoelekea katika hali ya utulivu lakini bila ya ufumbuzi kamili.
Hotuba ya Grandi katika mkutano wa 69 wa kamati kuu inakuja wakati idadi ya waliofurushwa makwao ikiongezeka na kufikia watu milioni 68.5 ambapo watu milioni 25. 4 kati yao wamesaka hifadhi nchi za ugenini ilhali milioni 40 ni wakimbizi wa ndani.
Ameongeza kuwa maelfu kadhaa wanaendelea kuvuka eneo la Sahel na baharí ya Mediteranea kuelekea Ulaya ambao wamekatishwa tamaa na kukabiliwa na ukatili pamoja na hatari zingine.
Grandi ameomba kuwepo na moyo wa kutoa hifadhi barani Ulaya akisema , kile kilichopewa jina la uokozi baharini kimetekwa na siasa.