Darfur ya sasa ni bora kuliko miaka 10 nyuma, lakini kazi bado ipo – Naibu Katibu Mkuu UN

28 Septemba 2018

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina Mohammed amesema hivi sasa jimbo la Darfur ya sasa nchini Sudan inaonekaana ni tofauti na Darfur ya miaka 10 iliyopita wakati ambapo Muungano wa Afrika, AU wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa pamoja walituma vikosi vya kulinda amani. 

Bi. Mohammed amesema hayo leo mjini New  York, Marekani wakati wa kikao cha kujadili kutoka ulinzi wa amani kuelekea ujenzi wa amani kwenye jimbo hilo ambalo liligubikwa na mapigano na sasa hali ni ya matumaini makubwa.

“Hii leo Darfur tunaona mapigano yakiiibuka katika milima ya Jebel Marra, lakini migogoro imepungua. Nje ya eneo hilo, mapigano yamepungua sana, na mapambano kati ya jamii na jamii yamepungua kwa kiasi kikubwa” anasema Bi. Amina Mohammed na kuongeza, “Haya ni mafanikio na hali ya wazi kuwa malengo yetu ya kunyamazisha bunduki barani Afrika linaweza kuwa jambo la kweli.”

Pia amesema wakati haya yakifanikiwa, baadhi ya mambo yaliyosababisha mgogoro zaidi ya miaka 15 iliyopita hayajazungumwa. “Ardhi na maliasili vinaendelea kutokuwekwa sawa. Watu wengi ambao wamejikuta wamekuwa wakimbizi katika nchi yao, hawajaweza kurejea katika makazi yao. Silaha bado zinaongezeka. Mkakati wa kusitisha mapigano bado unatakiwa kufikiwa. Na wapiganaji wa kikabila bado wanaendelea kuwa tishio.”

Aidha amesema kuwa inafahamika kuwa wakazi wa kawaida wa Darfur wanaendelea kukumbana na changamoto ngumu kabisa: ukiukwaji wa sheria, uhalifu, majanga ya kibinadamu, ukiukwaji wa haki za binadamu, unyanyasaji wa kijinsia, kutokuendelea kwa maendeleo endelevu, nafasi finyu ya kupata elimu, ukosefu wa nafasi za ajira na huduma za msingi za kijamii pia ukosefu wa utawala wa kisheria na huduma za usalama.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed akiwa ofisini kwake kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York
Picha UN News /Matt Wells
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed akiwa ofisini kwake kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York

“Watoto na vijana wadogo wamepoteza utoto wao kwa sababu ya machafuko.” Amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa “theluthi moja ya watu wanaendelea kuteseka kwa kukosa makazi wakiwamo wale wanaosalia ukimbizini nje ya nchi. Darfur inazidi kuwa imara lakini hatua hizo si imara, kuhakikisha hatua iliyofikiwa inaendelea si jambo jepesi.”

Naibu Katibu mkuu amesema hii ni kazi ngumu lakini ni muhimu kuvumilia. Kuendelea kwa mgogoro kutakuwa na athari kubwa kwa watu wa Darfur, ukanda wote na nje ya ukanda.

“Tunapambana kutoa huduma ya haraka kwa walio wakimbizi ndani ya nchi yao, kuwalinda wananchi, kuhamasisha kuheshimu haki za binadamu na kuwaewezesha na vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa amani” amesema Bi. Mohammed.

Aidha amesema wakati vikosi vya pamoja vya kulinda amani kutoka Muungano wa Afrika AU na Umoja wa Mataifa, UNAMID, vikijiandaa kuondoka Darfur, Umoja wa Mataifa utabaki bega kwa bega na watu na viongozi wa Sudan.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter