Hongera Sudan Kusini kwa kuchukua hatua zaidi kuwalinda watoto:Gamba

27 Septemba 2018

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto na migogoro ya Silaha, Bi. Virginia Gamba, ameipongeza serikali ya Sudan Kusini kwa kuongeza kipengele cha hiyari kwenye mkataba kuhusu haki za mtoto katika ushirikishaji kwenye migogoto ya kivita (OPAC).

Mabalozi wa Sudan Kusini, Bw. Kureng Garang na Agnes Oswaha waliongeza rasmi kipengele hicho kwenye hafla iliyofanyika kando ya mkutano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 jiji New York.

Bi. Gamba amesema “Leo hii serikali ya Sudan Kusini inatoa ahadi muhimu kwa watoto wake ya kwamba itachukua hatua zote kuwalinda na kuwaepusha kuajiriwa kama wanajeshi kwenye vikosi vya kijeshi na vikundi vyenye silaha nchini humo,”

OPAC pia unajumuisha ahadi kwamba serikali ya Sudan Kusini itafanya kazi ya kuondoa watoto wenye vyeo jeshini ambao wako chini ya umri wa miaka 18, na pia kkuwapa msaada wa kujikimu na kisaikolojia kabla ya kujumuishwa katika jamii.

Gaba amesema  anatumaini kuwa ahadi hii mpya ya kimataifa itatoa msukumo wa kimaendeleo kwa watoto wa Sudan Kusini, ikiwa ni pamoja na kutekeleza mpango uliorekebishwa wa kushughulikia masuala sita ambayo ni ukiukwaji mkubwa wa kibinaadamu dhidi ya watoto. Mwakilishi huyo maalum alikwenda Sudan Kusini mapema mwezi huu ili kujadili na serikali kuhusu suala hili na pia kuchagiza juhudi za kuwalinda vyema watoto.

Ameongeza kuwa  “Kupitia ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na pande kinzani nchini Sudan Kusini, tunaweka msingi wa kuboresha ulinzi wa wavulana na wasichana. Utekelezaji huu sasa utaleta maendeleo kwenye maisha ya watoto hao ambao wamekuwa waathirika au mashuhuda wa  vita vikali. Ninaishauri nchi ya Sudan Kusini ichukue hatua ya kutekeleza kanuni za Paris na Vancouver haraka iwezekanavyo,”

Sudan Kusini imekuwa nchi mwanachama ya 168 kushiriki katika kuongeza kipengele cha mkataba kuhusu ushirikishaji wa watoto katika migogoro ya kivita.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter