Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amehutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani huku akijinasibu kuwa wamebaini bohari la kisiri la silaha za atomiki nchini Iran lenye tani 300 za vifaa vya nyuklia.
Waziri Mkuu wa Israel akiwa amesimama katika mimbari ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ameonyesha picha ya kile anachodai ni pahali ambapo pamefichwa vifaa vya nyuklia huko Tehran, mji mkuu wa Iran.
Amedai kuwa “mwezi Mei tulifichua eneo kulikohifadhiwa mabaki ya siri ya mpango wa atomiki.Iko hapa. Katika kitongoji cha Shorabad cha mji wa Tehran. Leo nafichua eneo la pili la ghala la siri la atomiki ya Iran. Iko hapa, katika mtaa wa Turouzabad mjini tehran, umbali wa maili sita.”
Vile vile ameonyesha maeneo ambako anadai kuwa kumefichwa kile alichosema ni makombora ya Hezbollah karibu na uwanja wa ndege wa kimatifa wa Beirut nchini Lebanon.
Waziri Mkuu huyo wa Israel amesema “Hezbollah kimakusudi wanatumia raia wa Lebanon wasio na hatia , kama ngao. Wameweka makombora katika maeneo matatu karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut .”
Baadaye akaonyesha picha ya sehemu anayosema kumefichwa makombora hayo.
