Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Diplomasia ndio muarobaini wa kuondokana na nyuklia rasi ya Korea- Pompeo

Taswira  ndani ya ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mjadala kuhusu suala la kudhibiti kuenea kwa silaha za nyuklia huko Korea Kaskazini
UN /Loey Felipe
Taswira ndani ya ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mjadala kuhusu suala la kudhibiti kuenea kwa silaha za nyuklia huko Korea Kaskazini

Diplomasia ndio muarobaini wa kuondokana na nyuklia rasi ya Korea- Pompeo

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha ngazi ya mawaziri kujadili juhudi za kuondoa silaha za nyuklia zinazomilikiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK.

Mkutano huo ulioitishwa kwa mujibu wa kanuni  namba 37 za Baraza hilo umeongozwa na Waziri wa Mambo ya  Nje wa Marekani, Mike Pompeo kwa kuwa nchi yake ndio inashikilia urais wa chombo hicho kwa mwezi huu wa Septemba.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Bwana Pompeo amesema mwelekeo wa DPRK wa kuwa na mustakhbali wenye nuru unawezekana kwa njia ya diplomasia na kuondokana na silaha za nyuklia, “njia yoyote ile bila shaka itasababisha nchi hiyo kutengwa zaidi halikadhalika shinikizo.”

Katika kipindi cha mwezi huu cha uongozi wa Baraza la Usalama, Marekani imekuwa ikitilia mkazo masuala ya kudhibiti kuenea kwa silaha.

Bwana Pompeo amesema kuwa Rais Donald Trump wa Marekani ameweka bayana kuwa iwapo Rais wa DPRK Bwana Kim atazingatia ahadi basi mustakhbali bora waDPRK au Korea Kaskazini unakaribia.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Ye amepongeza uamuzi wa kisiasa wa DPRK au Korea Kaskazini na Korea Kusini kwa kusongesha maridhiano kati ya nchi zao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani  Mike Pompeo akizungumza wakati wa mjadala ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa silaha za nyuklia huko DPRK
UN /Loey Felipe
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo akizungumza wakati wa mjadala ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa silaha za nyuklia huko DPRK

Hata hivyo amesema anaamini kuwa mazunguzo ndio suluhu na kwamba mashinikizo hayana ukomo.

Urusi ikaangazia vikwazo vya mwendelezo wa kasi ya kutokomeza nyuklia kwenye rasi  ya Korea akisema ni ukosefu wa kuaminiana kati ya Marekani na DPRK ijulikanayo pia kama Korea Kaskazini. “Tunataka mfumo wa hakikisho wa kimataifa ambao unaweza kuwa na dhima mahsusi katika kutatua suala la kuondokana na nyuklia kwenye rasi ya Korea.

Hata hivyo amesema itakuwa si sahihi kwa nchi za magharibi kusaka kuimarisha vikwazo dhidi ya DPRK katika mazingira ya sasa ambamo kwayo kuna maendeleo ya kuondokana na silaha hizo.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini Kang Kyung-wha amesema maendeleo yaliyofikiwa kwenye rasi ya Korea hayakuweza kufikiriwa mwaka mmoaj uliopita. “Nchi yangu iko tayari kuendelea kufanya kazi na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama dhidi ya Korea Kaskazini vinatekelezwa huku ikiendelea kushirikiana na Korea Kaskazini katika kuwezesha maendeleo ya kina na hatimaye kuondokana kabisa na silaha za nyuklia.