Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tungearifiwa tungeshiriki mkutano leo kuhusu Afrika ya Kati:DRC

Wakimbizi wa DRC waelekea nchi zinginekufuatia vurugu. Picha: UNHCR

Tungearifiwa tungeshiriki mkutano leo kuhusu Afrika ya Kati:DRC

Amani na Usalama

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, imesema imeamua kutoshiriki mkutano maalumu wa ngazi ya juu wa mawaziri ulioandaliwa kandoni mwa mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu masuala yanayolighubika eneo la Afrika ya Kati ikiwemo DRC.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua hiyo ya DRC, Kikaya Bin Karubi mshauri wa Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo   amesema hawakuarifiwa mapema na wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani ambao ndio waandaaji wa mkutano huo uliopaswa kufanyika leo Alhamisi kwenye makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani

“Tulipofika hapa New York tuliambiwa kuwa kutakuwa na mkutano tarehe 27 (septemba 2018), mkutano unaoangalia masuala yote ya Afrika ya kati lakini hawakutuambia mapema kuwa kutakuwa na mkutano huo. Sisi tunaona hatuwezi kufika na twende katika mkutano kama ule na hatujui tunaenda kusema nini. Na tuliwaambia, kabla ya kuwaalika watu waje katika mkutano kama huo, ni lazima kama mtaongelea mambo yanayoihusu Congo ni lazima mapema kutuambia kwanza sisi na tusikilizane nao na tunaangalia malengo ni nini, tunataka kufikia nini na tutapata nini tukishamaliza huo mkutano. Rais Kabila, pia serikali ya Congo imesema hatuwezi kwenda katika mkutano huo, ni lazima tuangalie kama kunaweza kuwa na mkutano (mwingine) baadaye”

Na je kutohudhuria mkutano huu si ni kupoteza fursa adimu?

“Hapana tunakataa! Tunaona kama huu mkutano ni mtego. Kwa sababu gani sisi tuko Congo na tuna Waziri wetu wa mambo ya kigeni, kwa nini hawakutuandikia na kutuambia kwamba mtakapofika New York kutakuwa na mkutano utakaohusu Congo?! Tena mkutano unaohusu viongozi wa ngazi ya juu! Lakini hawakutwambia kitu chochote. Na hivyo sisi tumesema hatuwezi kwenda katika huo mkutano na nimesikia hautafanyika tena”

Na endapo taratibu zingefuatwa na wakahudhuria mkutano huo DRC ingekuwa na ujumbe gani?

“Tungeongelea mambo yote ya kuhusu DRC kama vile uchaguzi utakaofanyika mwezi wa 12, tungeangalia mambo ya usalama mashariki mwa DRC, Beni, unajua DRC kuna majeshi ya Umoja wa Mataifa MONUSCO, majeshi hayo yako kule miaka mingi sana!”