Ukosefu wa mazoezi wachochea magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

27 Septemba 2018

Kenya imesema inauchukulia kwa uzito wa juu mkutano wa leo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, NCDs, kutokana magonjwa hayo kuathiri baadhi ya wananchi wake.  

Waziri wa Afya wa Kenya Sicely Kariuki amesema hayo jijini New York Marekani akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa akisema kwamba…

 “Rais wetu Mheshimiwa Rais Uhuru ataungana na wenzake na kuzungumzia kwa kirefu vile ambavyo kila nchi itaendelea na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunatafuta uwekezaji na uwezeshaji wa kifedha ya kuelekeza kwa haya magonjwa ambayo katika dunia hatujaweka uzito vile inavyotakiwa”

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, magonjwa yasiyo yakuambukiza huua watu milioni 41 kila mwaka, sawa na asilimia 71 ya vifo vyote Duniani. Na waziri Kariuki anataja sababu ya kuongezeka kwa magonjwa hayo.

 “Watu wengi wanajikuta kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kwa vile Maisha yamebadilika, vyakula vimebadilika, hawatembei kama tulivyokuwa tunafanya nyakati za baba zetu na ndiyo tunataka sasa hivi tupambane na hayo kwa vile tukielewa ugonjwa kabla haujaendelea sana tunaweza kuushughulikia huo ugonjwa na watu wakarudi katika shughuli zao za kawaida”

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na kisukari, magonjwa ya akili, figo, pumu na saratani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter