Uhamiaji yafaa uwe salama na wa mpangalio: Guterres

Serikali, asasi za kiraia pamoja na mamlaka za kikanda zimehimizwa kujitayarisha vyema kwa mkutano mkuu kuhusu uhamiaji zikiwa tayari kuweka azma kuwa zitatumia faida za uhamiaji uliosimamiwa vizuri kwa minajili ya kupunguza athari mbaya za sera mbovu na kutokuwepo ushirikiano katika suala zima la uhamiaji.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Antonio Guterres, amesema hayo leo katika hotuba yake kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhus uhamiaji jijini New York, Marekani, mkutano uliopatiwa jina “mwelekeo hadi Marrakesh,” ambako kutafanyika mkutano wa kimataifa wa uhamiaji.
Bwana Guterres amesema mkataba wa kimataifa kuhusu uhamiaji utarahisisha uhamiaji wa aina yote ili uwe, “ salama , wenye mpangilio na wenye kuondoa adha.”
Amesema kuwa suala la uhamiaji linamhusu kila mtu na kuongeza kuwa, athari zake za kiuchumi zinagusa hata kampuni na mashirika makubwa ya kimataifa.
Akiendelea kuumwagia sifa mpango mpya kuhusu uhamiaji , Bw Guterres akisema unatilia mkazo haja ya ushirikiano katika juhudi za kushughulikia suala hilo na kuongeza kuwa unatambua kuwa mbali na kila taifa linawajibika na kile kilichoko ndani ya mpaka wake, lakini duniani hii ya kutegemeana inahitaji ufumbuzi ulioegemea ushirikiano na kufuata yale ambayo yanafanana.
Katibu Mkuu amesema ameanzisha mtandao mpya wa uhamiaji ndani mwa Umoja wa Mataifa ili kuunga mkono mataifa wanachama katika utekelezaji wa mkataba wa uhamiaji akisema mkataba huo utasaidiwa kwa karibu na shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM.
Kwa sasa inakadiriwa kuwa kuna wahamiaji milioni 260 duniani ambapo nusu yao ni wanawake na wasichana ambapo Guterres amesema, “utekelezaji wa mkataba wa uhamiaji unapaswa kusikiliza sauti na mahitaij yao.”
Naye rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bi. María Fernanda Espinosa, amesema kuwa, wakati huu suala la uhamiaji limeigawanya dunia kutokana na athari zake kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Ameongeza kuwa ingawa hawawezi kurudisha nyuma yaliyopita, amesema ni wakati wa kuganga yajayo na kusema wanaweza kubadili ya hapo baadaye.
Amesema kuwa ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kupiga tochi katika hali ya usoni na kutafakari jinsi ya kulishughulikia na kusema kuwa kwa kufanya hivyo ni sharti kuzingatia kuwa ingawa uhamiaji hutoa nafasi sawa kwa wahamiaji na wenyeji, lakini wale wanaopinga uhamiaji huenda hutizama tu changamoto za ukweli au za kudhaniwa.