Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Imani imetoweka duniani, ushirikiano wa kimataifa nao mashakani- Kenya

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN, New York, Marekani
UN/Cia Pak
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la UN, New York, Marekani

Imani imetoweka duniani, ushirikiano wa kimataifa nao mashakani- Kenya

Amani na Usalama

Ongezeko la uelewa wa wananchi kuhusu rasilimali zilizopo na huduma wanazopata kutoka kwenye serikali zao ni moja ya mambo yaliyotajwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kuwa yanasababisha wananchi kukosa imani na taasisi zao zinazowaongoza.

Akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo mjini New York, Marekani, Rais Kenyatta amesema wananchi kwa uelewa wa uwepo rasilimali hizo, sambamba na kushamiri kwa vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya mali za umma, wanazidi kupoteza imani kwa serikali zao.

“Mifumo  mibaya ya utawala inatumika hovyo kwa maslahi ya wachache huku mwananchi wa kawaida akiumia. Vyombo huru vya habari na mitandao ya kijamii vimesheheni habari kuhusu ulaghai na mipango ya kifedha ambayo inabinafsisha faida wakati wa ustawi na kueneza kwa wananchi hasara inapopatikana,” amesema Rais Kenyatta.

UNNewsKiswahili/Assumpta Massoi
Rais Kenyatta katika #UNGA73

 “Naamini jukumu la dharura la kisiasa duniani hivi sasa ni kufunga pengo hili la imani kati ya wananchi na taasisi zinazowaongoza. Serikali zinadaiwa imani na wananchi, na iman ihiyo lazima ipatikane na ilindwe,” amesema Rais Kenyatta akiongeza kuwa “ si kwamba naongeza chumvi ya kwamba suala hili linahusika na mustakhbali wa utulivu duniani na mwendelezo wa uwepo wa serikali.”

Rais huyo wa Kenya pia amezungumzia hali ya kimataifa hususan ushirikiano wa kimataifa akisema kuwa katu ushirikiano huo haujawahi kuwa kwenye tishio kubwa kama sasa. Amesema mwenendo wa biashara duniani na usimamizi wa mfumo wa kiuchumi ni viashiria vya jinsi hali ya ushirikiano wa kimataifa ilivyo.

Amegusia pia ushirikiano wa Kenya na Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa utaendelea kuimarishwa huku akiomba Umoja wa Mataifa na wadau waendelee kusaidia harakati za amani akitaja nchi kama Sudan Kusini ambayo amesema Kenya imewakua nao sambamba katika safari ya amani pamoja na Sudan.