Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wa sasa si wa kusubiri kufunguliwa milango- Rais Ramaphosa

Rais Matamela Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo tarehe 25 Septemba 2018
UN/Cia Pak
Rais Matamela Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo tarehe 25 Septemba 2018

Vijana wa sasa si wa kusubiri kufunguliwa milango- Rais Ramaphosa

Ukuaji wa Kiuchumi

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amehutubia mjadala mkuu wa Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa ikiwa ni mara ya kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa huo akisema kuwa vijana wa sasa si wale wa kusubiri kufunguliwa milango.

Amesema vijana wa sasa Afrika wako tayari kubadilisha bara lao liwe bora zaidi kwa kuzingatia changamoto za maendeleo zinazokabili bara lao, akiongeza kuwa huu ni wakati wao na huu ni  mwaka wao, “ hebu tuwaache wachanue kwa kadri ya uwezo wao.”

“Ikiwa ni bara ambalo lina idadi kubwa zaidi ya vijana duniani, Afrika ina uwezo wa kukua na kuibuka lango lijalo la ukuaji wa uchumi duniani,” amesema Rais Ramaphosa.

Vijana wa sasa Afrika si wa kusubiri kufunguliwa milango. Hebu na tuwaache wachanue kwa kadri ya uwezo wao

Akimnukuu Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, hayati Mzee Nelson Mandela, Rais Ramaphosa amesema “ wakati mwingine inakuwa ni jukumu la kizazi kimoja kugeuza jamii kuwa bora zaidi.”

Hata hivyo amesema Afrika hivi sasa “tunahaha kunyamazisha bunduki ifikapo mwaka 2020 ili kuondokana na mizozo ambayo imegharimu maisha ya mamilioni ya watu wetu, wengine wengi wamesalia wakimbizi na kudumaza ukuaji wa kiuchumi.”

Rais Ramaphosa amesema Afrika iliyo imara inawezekana kwa kuwekeza kwenye elimu sahihi, kuboresha afya, utawala bora na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.